Habari

Kenya Power ichunguzwe kwa kuwapunja Wakenya – Wabunge

April 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MHASIBU Mkuu wa serikali Edward Ouko ametakiwa kuufanyia ukaguzi mfumo ambao hutumiwa na kampuni ya kusambaza umeme Nchini, Kenya Power, kutengeneza ada za umeme, maarufu tokens.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) Jumanne alisema wanachama wa kamati hiyo wameelezea hofu kwamba huenda kampuni hiyo inawapunja wateja wa umeme mamilioni ya pesa kupitia mfumo huo.

“Tutataka kujua jinsi zabuni ya “tokens” hutolewa na kufuatilia habari kuhusu kampuni ambazo hupewa zabuni hiyo kubaini ikiwa zinahitimu kutoa huduma hizo,” akasema Bw Nassir.

Alisema ingawa suala hilo halijaibuliwa kwenye ripoti ya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika Kenya Power ambayo kamati hupiga msasa wakati huu kufungamana na wajibu wake, ukaguzi huo unafaa kwa sababu wananchi wamekuwa wakilalamikia suala hilo.

Wakuu wa Kenya Power walikuwa wameratibiwa kufika mbele ya PIC Jumanne lakini wakaomba kikao hicho kiahirishwe ili kuwaruhusu kushughulikia masuala mengine ya dharura.

Katika muda wa mwezi mmoja uliopita, kampuni hiyo ambayo ina ukiritimba wa kusambaza umeme nchini imekuwa ikilaumiwa kwa kuwapa wateja wake bili za juu za umeme; wateja wanaolipa baada ya kutumia stima.

Na wale wanalipia umeme kabla ya kutumia chini ya mfumo wa “tokens” pia wamekuwa wakilalamikia ufanisi wa huduma hiyo baadhi wakidai kucheleweshwa kwa stima baada ya mteja kununua “tokens”.

Kenya Power pia imekuwa ikilaumiwa kutoa zabuni kwa kampuni zingine za kuuza “tokens” ambazo huwatoza watumiaji stima ada za juu kuliko “tokens” ambazo Kenya Power” huuza moja kwa moja kwa wateja hao hao.

Kampuni ambazo zimekuwa zikipewa kandarasi hiyo na Kenya Power ni kama vile; Vendlt na Dynamo Digital ambazo hutoza ada za juu kwa “tokens” kuliko zile ambazo hununuliwa kutoka kwa Kenya Power kupitia nambari ya malipo (Pay Bill) ya M-Pesa ya 888880.

“Mimi pia ni mwathiriwa. Nakumbuka nyumbani kwangu tulikumbwa na hitilafu hii. Ilitulazimu kumpigia simu afisa mmoja wa ngazi ya juu wa KP kutaka atupe maelezo kuhusu chanzo cha shida hizo,” akasema Bw Nassir

Afisa Mkuu Mtendaji Ken Tarus Jumatatu alisema kuwa asilimia 85 ya “tokens” hununuliwa kupitia “Pay Bill no” ya Kenya Power, hali ambayo husababisha msongamano ambao huchukua muda kumalizwa.

Lakini wakati wa msimu wa Sikuu Kuu ya Pasaka, huduma ya “tokens” ilicheleweshwa kwa hadi saa 24.

Mapema wiki hii kampuni hiyo iliwaarifu wateja wake kwamba huduma ya “tokens” haitakuwepo katika ya saa nne usiku  Jumanne na saa kumi na mbili asubuhi Jumatano asubuhi.

Kampuni hiyo vile vile ilisema kuwa ongezeko la ada ya stima na hitalifa kuhusu “tokens” zilitokana na uhamiaji wa utozaji wa ada ya stima kutoka mfumo wa zamani hadi mfumo mpya.

Hata hivyo, hadi wakati ambapo shughuli hiyo ilikamilishwa, wateja wengi walikuwa tayari wameathirika pakubwa kwa kukosa nguvu za umeme nyumbani na katika biashara zao.