HabariKimataifa

Kenya yapata kiti muhimu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA AGGREY MUTAMBO

KENYA imepata kiti muhimu cha uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuishinda Djibouti katika awamu ya pili ya kupiga kura Alhamisi.

Kinyang’anyiro baina ya Kenya na Djibouti kililazimika kuendelea kwa siku ya pili baada ya awamu ya kwanza hapo Jumatano kukosa mshindi, Kenya ilipozoa kura 113 dhidi ya 78 za Djibouti, huku idadi ya kura zinazohitajika kutawazwa mshindi ikiwa 128.

Lakini Alhamisi, Kenya ipigiwa kura na mataifa 129 huku nchi zilizopigia Djibouti zikipungua hadi 62. Ili kupata kiti hicho, taifa linalowania linafaa kupata kura 128, ambazo ni thuluthi mbili ya mataifa yote 193, kulingana na sheria za baraza hilo.

Hii inamaanisha kuwa kuanzia Januari 2021, Kenya itarejelea uwepo wake katika asasi hiyo ya Umoja wa Mataifa baada ya miaka 23, ambapo itasaidia kufanya maamuzi muhimu kuhusu usalama na amani duniani. India, Mexico, Ireland na Norway zilichaguliwa hapo Jumatano.

Baadhi ya maamuzi ambayo Kenya sasa itashiriki ni kuhusu kupiga mataifa marufuku kama adhabu, kutoa kibali cha kutumia majeshi kudumisha amani pamoja na kuchagua majaji wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki.

Kenya sasa itashirikiana na wanachama watano wa kudumu wa baraza hilo – Amerika, Urusi, Uingereza, Uchina na Ufaransa, pamoja na wanachama wengine tisa wasio wa kudumu,. na huenda hata itakapata fursa ya kusimamia vikao vya baraza hilo.

Kenya ilikuwa imependekezwa na Umoja wa Afrika kwa nafasi hiyo, nayo Djobouti ikajitokeza kama mshindani.

Alhamisi, uchaguzi huo ulianza saa kumi alasiri ambapo Venezuela ilizuiwa kupiga kura kutokana na uanachama wake kukosa kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa. Matokeo hayo yalitangazwa saa mbili usiku.

Kenya ilitumia kila mbinu kutwaa ushindi kwa kushawishi mataifa mengi kuipigia kura. Iliteua Bw Tom Amolo, Katibu wa Ubalozi na Siasa kama balozi wake maalumu, akisaidiwa na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika Bi Catherine Mwangi na Bw Lazarus Amayo, Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa jijini New York.

Kenya pia ilialika wawakilishi wengi humu nchini kutoka mataifa ya nje, na kuwashawishi kuipigia debe katika kila kongomano la kimataifa kabla ya ugonjwa wa Covid-19.

Ingawa juhudi hizo ziligharimu hela nyingi, kilikuwa kiti ambacho Kenya haikutaka kupoteza maanake jitihada za hivi majuzi za kutwaa uongozi katika ngazi za kimataifa zimekuwa zikigonga mwamba.

Nairobi ilikuwa imepoteza fursa ya kuwa makao ya ukatibu wa Eneo Huru la Biashara la Afrika, nafasi iliyotwaliwa na Ghana. Pia ilipoteza nafasi ya kiongozi wake kuchukua hatamu za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Pia ilikosa kuteuliwa kuwa makao makuu ya benki ya Afrexim.