HabariHabari za Kitaifa

Kesi ya kuandamana hadi ikulu yaambulia patupu

Na JOSEPH WANGUI November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WANAHARAKATI wamepoteza kesi ya kutaka wananchi waruhusiwe kufanya maandamano nje ya Ikulu na ikulu ndogo ya Rais katika maeneo mbalimbali nchini.

Mahakama ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na kundi la Operation Linda Jamii, ikisema halikuthibitisha jinsi notisi zilizotangaza makazi hayo kuwa maeneo yaliyolindwa zinavyokiuka Katiba au sheria.

Notisi hizo zinajumuisha Ikulu za Nairobi na Mombasa pamoja na ikulu ndogo za Kisumu, Sagana, Nyeri, Eldoret, Nakuru na Kisii.

Wanaharakati walidai kuwa marufuku hiyo inakiuka haki ya wananchi kukusanyika, kuandamana na kuwasilisha malalamishi yao kwa Rais William Ruto.

Hata hivyo, mahakama ilisema Sheria ya Maeneo Yanayolindwa haizuii watu kuingia kabisa, bali inadhibiti kuingia kwa kutaka kibali kutoka kwa maafisa walioidhinishwa.

“Kuingia katika maeneo hayo hakujapigwa marufuku, bali kunadhibitiwa,” ikasema mahakama.

Iliongeza kuwa wananchi wanaweza kuwasilisha malalamishi yao katika afisi nyingine za serikali, ikiwemo Afisi ya Rais, bila kulazimika kufika ikulu au ikulu ndogo.