HabariHabari za Kitaifa

Wakenya walivyotekeleza ulaghai wa Sh25bn pesa za Amerika

Na HILLARY KIMUYU November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MKENYA aliyepata kadi ya kuishi Amerika, Green Card, kupitia bahati nasibu mnamo 2024 anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika ulaghai wa Sh25.8 bilioni uliolenga fedha za serikali za kuwasaidia wanafunzi kugharimia elimu ya juu.

Francis Smith Mogambi anadaiwa kushirikiana na washirika wake nchini Kenya kati ya Novemba 2025 na Mei 2026 kuiba taarifa za kibinafsi za raia wa Amerika na kuzitumia kuwaandikisha katika vyuo vya mtandaoni bila wao kujua.

Washukiwa walitumia taarifa hizo kuwasilisha maombi ya mikopo na misaada ya elimu kupitia mpango wa serikali wa FAFSA. Baada ya fedha kutolewa, walidaiwa kuzichukua kupitia akaunti za benki na hundi bandia.

Mogambi anadaiwa kupokea hundi zilizoandikwa kwa majina ya wanafunzi hewa, kuzitia saini na kuweka fedha hizo katika akaunti zake. Inadaiwa alisalia na asilimia 30 na kisha kutuma nyingine kwa washirika wake Kenya.

Polisi walianza kumchunguza baada ya shahidi kusema alijaribu kumshawishi kujiunga na ulaghai huo kwa kumwahidi dola 2,000 (Sh259,000) kila wiki.

Mnamo Oktoba 19, Mahakama kuu Nebraska ilimfungulia mashtaka 10, yakiwemo ya kuiba fedha za serikali na kutumia utambulisho wa watu wengine.

Uchunguzi huo, uliopewa jina la ‘Operation Ghostbusters’, pia umehusisha washukiwa katika New Jersey na Virginia.

Serikali za Kenya na Amerika zinazuia sarafu za kidijitali zenye thamani ya dola 750,000 (Sh97.4 milioni) zinazohusishwa na ulaghai huo.

Ushirikiano huo unahusisha asasi za usalama na haki kama DCI, ARA, ODPP, KRA na FRC. Maafisa wa Amerika pia wamejadiliana na Kenya uwezekano wa kuwarejesha washukiwa nchini Amerika kukabili mashtaka.

“Hundi hizo zilitolewa kwa majina ya wanafunzi tofauti, lakini zote zilikuwa na sahihi zilizomlipa Mogambi,” polisi walisema katika hati ya kiapo.