Kimataifa

Aibu mbunge akiwapa wakazi majembe wamchague tena

Na GODFREY MASIKO, Daily Monitor March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa eneobunge la Kagoma, Wilaya ya Jinja, Mashariki mwa Uganda wamekataa majembe waliotunukiwa na Mbunge wao Moses Walyomu Muwanika aliyedai wanahitaji vifaa hivyo katika msimu huu wa upanzi.

Pia, mbunge huyo aliwazawadi majembe hayo kama kishawishi cha kuwavutia wampigie kura katika uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao, 2026.

“Sio mimi pekee yangu niliyekataa jembe kutoka kwa mbunge huyo, wakazi wengi pia walikataa. Tumechoka kupewa majembe kila uchaguzi unapokaribia. Tunahitaji usaidizi wa maana. Mbona huwa anatupa majembe kila mara? Jembe moja baada ya miaka mitatu, haitoshi. Achukue majembe yake,” mmoja wa wakazi, Bw Denis Kafuko, akasema.

Kulingana na Bw Kafuko, mbunge huyo hutembelea eneo hilo wakilishi uchaguzi unapokaribia na hupotea nyakati zingine.

“Mbunge wetu hatujali kwamba hujitokeza tu msimu wa kampeni. Tumechoka na tunataka ajue kuwa hatujaridhishwa na utendakazi wake. Tumeendelea na maisha yetu kwa miaka mitatu bila usaidizi wake, na tuna imani kwamba tunaweza kukamilisha muhula huu bila usaidizi wake,” akasema.

Bi Amina Naigaga, mkazi wa kijiji cha Itakaibolu, alishangaa ni vipi mbunge huyo ameanza kusambaza majembe kabla ya kufanya mashauriano nao.

“Awali, ilikuwa ni sawa, lakini wakati huu nani alimuitisha majembe? Mahitaji yetu hubadilika kila wakati, zamani tulihitaji majembe sasa hatuyahitaji,” akasema.

“Familia zote huwa hazitegemei kilimo, mahitaji yetu yanaweza kubadilika mwaka hadi mwingine,” Bi Naigaga akaongeza.

Kulingana na mama huyo, wanasiasa hufanya makosa kwa kutofuatilia mahitaji ya wakazi wa maeneo wanayowakilisha.

Imekuwa kawaida kwa wanasiasa wanaomezea mate viti vya kisiasa kama ubunge kuwasambazia raia aina mbalimbali za zawadi watika uungwaji mkono.

Vitu ambavyo wanasiasa hutoa nyakati kama hizo ni pamoja na majembe, fulana, baiskeli, aina mbalimbali za vyakula, pesa, miongoni mwa vingine.

Zawadi kama hizo pia huchukuliwa kama hongo za kuwashawishi wakazi kumpigia kura mwanasiasa anayezitoa.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga