Amerika yazima ufadhiliwa wa Sh1.7 bilioni kwa kikosi cha amani Haiti
AMERIKA imezima ufadhili wa kima cha dola 13 milioni (Sh1.7 bilioni) kwa kikosi cha walinda usalama kutoka mataifa mbalimbali (MSM), kikiongozwa na Kenya, kinachoendesha operesheni za kurejesha amani Haiti, Umoja wa Mataifa ulithibitisha Jumanne.
Hii ni kufuatia amri ya Rais Donald Trump kwamba Amerika ikatize misaada ya kigeni kwa miezi 90 “kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusu manufaa ya mipango hiyo.”
“Amerika ilikuwa imeahidi kutoa dola milioni 15 (Sh1.95 bilioni), dola 1.7 milioni (Sh22 milioni) kati ya hizo zilikuwa zimetumwa kwa hazina maalum ya UN kwa ufadhili wa shughuli za kupambana na wahalifu Haiti, kwa hivyo dola 13.3 milioni (Sh1.729 bilioni) sasa zimezuiwa,” msemaji wa UN Stephane Dujarric aliwaambia wanahabari.
“Tumepokea ilani rasmi kutoka Amerika kwamba mchango wao umesitishwa,” akaongeza.
Kikosi cha walinda usalama, kinachoshirikisha polisi 627 wa Kenya, kilitumwa Haiti mwaka jana kusaidiana na polisi wa nchi hiyo kurejesha amani kwa kupambana na magenge ya uhalifu. Kutumwa kwa walinda usalama hao kuliidhinishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa (UNSC) mnamo Oktoba 2023, japo hicho sicho kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Kwa hivyo, ufadhili wa walinda usalama hao unategemea michango ya hiari kutoka mataifa mbalimbali ya ulimwengu, ambayo umekuwa finyu.
Zaidi ya dola 110 milioni (Sh14.3 bilioni) zimetumwa kwa hazina maalum ya UN ya kusaidia kikosi hicho— kiasi kikubwa cha pesa hizo kikitoka Canada.
Hazina hiyo iliundwa kutokana na msukumo wa Amerika kuhimiza mataifa wanachama wa UN kuchangia. Lakini nchi nyingi zimejivuta kutoa michango yao, zikidai kulemewa na mzigo wa utoaji misaada.
Kwa hivyo, kikosi hicho cha walinda usalama hakijakuwa kikipata ufadhili wa kutosha, hakina vifaa tosha na kinakabiliwa na uhaba wa maafisa wa kutosha.
Wakati huu kikosi hicho cha MSM kina jumla ya polisi na wanajeshi 900 pekee badala ya jumla ya walinda usalama 2, 500 wanaohitajika.
Walinda usalama hao 900 wanatoka Kenya, El Salvado, Jamaica, Guatemala na Belize.
Mnamo Jumanne wiki jana, wanajeshi 70 wa Salvador waliwasili jijini Port-au-Prince, Haiti, japo wajibu wao sio kukabiliana na wahalifu.
Wao ni wataalamu wa kuwasafirisha kwa ndege waliojeruhiwa katika makabiliano.
Saa chache baada ya kuingia mamlakani Januari 20, 2025, Rais Trump alitia saini agizo la kusitisha, mara moja, misaada yoyote ya kigeni kutoa nafasi kwa ukaguzi ndani ya siku 90.
Hatua hiyo iliathiri mipango ya afya na usalama, kote ulimwenguni ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Amerika.
Nchini Kenya, inakadiriwa kuwa jumla ya watu 35,000 wamepoteza ajira katika miradi na mipango mbalimbali, haswa na kiafya, ambayo imekuwa ikifadhili na Amerika kwa muda mrefu.