Biden akataa kujitoa mbio za urais Amerika licha ya hofu ya kulemewa na uzee
WASHINGTON DC, Amerika
RAIS wa Amerika Joe Biden ameapa kuendelea kupambana katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa urais ili kuwatuliza wafuasi wa chama chake cha Democratic na washirika wakuu. Hii ni baada ya kukubali kulemewa kwenye mjadala kati yake na Donald Trump wiki iliyopita.
Wakati wa mahojiano na kituo cha radio nchini humo, alikiri kufanya kosa akiwataka wapigakura kukosa kumhukumu wakati yupo katika Ikulu ya White House.
Jumatano, ripoti zilidokeza kwamba Bw Biden alikuwa akitathmini mustakabali wake, kuwatuliza wafuasi wake, wakiwemo magavana wa majimbo na wafanyakazi wa kampeni yake.
Bw Biden aliweka wazi kuwa atasalia kwenye kinyang’anyiro hicho na Bi Harris akasisitiza kumuunga mkono.
“Mimi ndiye mteule wa Chama cha Democratic. Hakuna mtu wa kuniondoa. Siondoki,” alisema Bw Biden.
Naibu wa Rais Kamala Harris ameonekana kumuunga Biden baada ya uvumi kuenea kuwa Bi Harris angechukua nafasi yake kama mgombea urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.
“Wacha niseme haya kwa uwazi na kwa urahisi. Ninagombea na nitakuwa kwenye kinyang’anyiro hicho hadi mwisho,” alisisitiza Bw Biden.
Maswali yamekuwa yakiibuka iwapo Bw Biden, 81, ataendelea na kampeni yake kufuatia mjadala na Trump, uliozua wasiwasi katika chama cha Democratic kuhusu uwezo wake kushinda uchaguzi huo.
Shinikizo za kumtaka Bw Biden kubanduka zimeongezeka siku chache kutokana na kura nyingi zinazoonyesha kuwa mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump anazidi kupata umaarufu.
Kura ya maoni ya New York Times iliyofanywa baada ya mjadala huo, ilionyesha kuwa Trump alikuwa akishikilia uongozi kwa mbali zaidi kwa alama sita.