Kimataifa

Bobi kwa Museveni: Nitakulinda ikiwa utaachilia mamlaka kwa amani

Na MASHIRIKA, WINNIE ONYANDO October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, amesema Rais Museveni atalindwa iwapo atakabidhi madaraka kwa amani.

Akiwahutubia wafuasi wake katika uwanja wa michezo wa Busubizi katika Wilaya ya Mityana jana, Bw Kyagulanyi alisema wakazi wa taifa hilo wataendelea kuteseka ikiwa Museveni atasalia mamlakani.

“Ikiwa Museveni atakabidhi madaraka kwa amani, tutamlinda,” alisema.

Kyagulanyi aliwarai wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya kuiondoa serikali ya NRM madarakani ifikapo Januari 2026.

“Barabara zetu hapa ni mbovu, wakazi hawapati huduma bora, lakini kwa sasa, sitazungumza sana kuhusu hili kwa sababu watasema mimi ni mkabila, lakini hili ndilo eneo lililompa Museveni kura nyingi.”

“Mishahara ya walimu itakuwa kipaumbele mara tu tutakapoingia madarakani,” akaongeza Bobi Wine.