COVID-19: Amerika yashauri raia wake waepuke Kenya ikiwezekana
Na BENSON MATHEKA
AMERIKA imeonya raia wake dhidi ya kutembelea Kenya ikisema kwamba wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa virusi vya corona.
Kinaya ni kwamba visa vya maambukizi katika nchi hiyo vinaongezeka kuliko Kenya na inaongoza kwa vifo vinavyosababishwa na virusi hivyo ulimwenguni.
Onyo hilo lililotolewa Alhamisi, Agosti 6, 2020, linawataka raia wa Amerika kuwa waangalifu wasiambukizwe corona na kuepuka vitendo vya kigaidi na utekaji nyara wakiwa Kenya
“Fikiria kubadilisha safari yako Kenya kwa sababu ya Covid-19. Kuwa mwangalifu ukiwa Kenya kwa sababu ya uhalifu, ugaidi, masuala ya afya na utekaji nyara. Baadhi ya maeneo ni hatari sana,” linasema onyo la kiwango cha tatu lililotolewa na kituo cha kuzuia maradhi cha Amerika.
Kwenye onyo hilo, Amerika inataja kulegezwa kwa masharti ya kuzuia kusambaa kwa corona kulikotangazwa na serikali ya Kenya na kurejelewa kwa shughuli za uchukuzi wa umma na biashara.
Rais Uhuru Kenyatta alilegeza masharti hayo Julai 6, 2020, na idadi ya maambukizi na vifo vimeendelea kuongezeka.
Amerika ina visa zaidi ya 5 milioni vya corona na vifo 162,441 ikilinganishwa na visa 25,000 na vifo 420 nchini Kenya.
Nchi hiyo iliwahimiza raia wake kutotembelea maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Kenya na Somalia na miji ya Pwani ya Kenya licha ya visa vya ugaidi kutoripotiwa majuzi.
Iliwaonya dhidi ya kutembelea Kaunti ya Turkana na mitaa ya Eastleigh na Kibera jijini Nairobi ikisema kuna hatari ya kutekwa nyara.
“Uhalifu wa kimabavu kama utekaji nyara, kukamatwa ngeta, kuvunjwa kwa nyumba na utekaji nyara unaweza kutokea wakati wowote. Polisi wanajitolea kusaidia lakini hawana uwezo wa kukabili visa vya uhalifu mkubwa na mashambulizi ya kigaidi. Huduma za dharura za afya na kuzima moto ni duni,” inasema serikali ya Amerika kwa raia wake.
Onyo hilo limejiri wakati sekta ya utalii imeanza kufufuka baada ya serikali kuondoa marufuku ya safari za ndege za kimataifa.
Nchi hiyo pia imeonya raia wake walio Uganda na Tanzania kwamba wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa corona.