Hali tete Cameroon, matokeo ya urais yakitangazwa hii leo
UTATA mkubwa wa kisiasa unanukia Cameroon huku Tume ya Uchaguzi Nchini ikitarajiwa kutangaza mshindi wa kura za urais leo.
Mnamo Jumatano, Mahakama ya Kikatiba ya Cameroon ilitupilia mbali kesi zote zilizowasilishwa kuanika udanganyifu na wizi wa kura uliodaiwa kutokea kwenye uchaguzi ulioandaliwa majuma mawili yaliyopita.
Rais Paul Biya, 92 ambaye anasaka muhula wa nne madarakani, takwimu zinaonyesha yupo kifua mbele dhidi ya Kiongozi wa upinzani Issa Tchiroma.
Ghasia tayari zilianza kushuhudiwa kaskazini mwa Cameroon ambako Tchiroma ana uungwaji mkono mkubwa.
Wafuasi wake walikabiliana na maafisa wa usalama huku Tchiroma mwenyewe kwenye ukurasa wa Facebook akijitangaza mshindi wa rais na kusema anasubiri kupokezwa mamlaka kwa njia ya amani.
Tchiroma ambaye alikuwa mwandani wa Biya, alidai kuwa ameshinda uchaguzi kwa asilimia 54.8 baada ya asilimia 80 ya kura kuhesabiwa.
Kiongozi huyo hata hivyo si kati ya wale ambao waliwasilisha kesi mahakamani lakini alionya kuwa hatakubali apokonywe ‘ushindi’ wake.
“Iwapo tume itatangaza matokeo ambayo yameghushiwa, itakuwa imechezea imani ya raia na sote tutapambana hadi tupewe ushindi wetu,” akasema Tchiroma.
Mahakama ilitupilia mbali kesi 10 ambazo zilidai wapigakura walitishiwa na kura kuibwa ikisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha.
Serikali nayo ilikanusha madai ya kuwa imeshiriki wizi wa kura na kuwataka raia wa Cameroon watulie hadi mshindi wa uchaguzi huo atangazwe.
Baada ya matokeo ya awali kuonyesha kwamba Biya alikuwa kifua mbele, maandamano yalianza kushuhudiwa kwenye baadhi ya miji kama Maroua na Garoua.
Iwapo Biya atatangazwa mshindi, basi atakuwa madarakani kwa miaka saba zaidi.
Hiyo nayo itakuwa na maana kuwa akifanikiwa kumaliza muhula wake, atakuwa ametimu umri wa takriban miaka 100.
Mwalimu mmoja aliuawa baada ya kupigwa risasi wakati wa maandamano Garoua ambako wafuasi wa upinzani walikuwa wakibeba mabango yenye jina la Tchiroma,74.