Harris akubali kushindwa, ampongeza Trump
WASHINGTON DC, AMERIKA
MAKAMU wa nchini Amerika ambaye alikuwa mgombea urais wa chama cha Democratic Kamala Harris amekubali kushindwa na Donald Trump na amewataka wafuasi wake kuendelea kutetea maono ya maendeleo ya nchi hiyo.
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika Chuo Kikuu cha Howard mjini Washington Jumatano jioni, baada ya Trump kupata zaidi ya kura 270 za majimbo zinazohitajika kushinda kwenye uchaguzi wa urais, Harris aliwahimiza wafuasi wake kutokata tamaa.
Trump alirejea kisiasa kwa namna ya kushangaza, miaka minne baada ya kukataa kukubali kushindwa, jambo lililosababisha machafuko na vurugu katika makao ya serikali ya Amerika.
“Nakubali kushindwa katika uchaguzi huu, lakini sikubali kushindwa kwa mapambano yaliyochochea kampeni hii,” alisema Harris.
“Nisikilizeni ninaposema mwanga wa ahadi ya Amerika utaendelea kung’aa, mradi tusikate tamaa kamwe,” aliongeza sauti yake ikiwa imekauka baada ya kampeni kali zilizochukua wiki 13.
Wakati huo huo, Harris alimpigia simu Trump kumpongeza kwa ushindi wake baada ya kuchaguliwa tena kuongoza taifa hilo.
Aliongeza kuwa yeye (Harris) na Rais Joe Biden watasaidia kufanikisha mabadiliko ya mamlaka kwa njia ya amani.
Katika hatua nyingine, Rais Biden pia alizungumza na rais mteule Trump kwa njia ya simu ambapo alimpongeza kwa ushindi alioupata kwenye uchaguzi wa Novemba 5 na kumkaribisha kuitembelea ikulu ya White House akijiandaa kuchukua hatamu za uongozi.
Kukubali hadharani kwa makamu huyo wa rais kulimaanisha mwisho wa mchakato wa uchaguzi uliodumu kwa zaidi ya siku 100.
Trump alishinda uchaguzi wa Jumanne na kuwa rais wa 47 wa nchi hiyo huku akitwaa takriban majimbo matano kati ya saba muhimu yenye ushindani.
Trump na makamu wake JD Vance, wataingia madarakani Januari 20, 2025 kwa muhula wa miaka minne.