Kimataifa

Hofu huenda Putin ana siri kali ya kusaidia Trump kutwaa urais Amerika

Na MASHIRIKA October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON, AMERIKA

ALIYEKUWA Rais wa Amerika Donald Trump ameongea na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mara saba tangu aondoke mamlakani, mwanahabari nguli wa Amerika amedai.

Mwanahabari huyo Bob Woodward kwenye kitabu chake chenye mada ‘Vita’ amesema kuwa Trump na Urusi ni marafiki wakubwa.

Anadai wawili hao wamekuwa wakizungumza hata baada ya rais huyo wa zamani kushindwa kwenye uchaguzi wa mnamo 2022 na akaondoka afisini mnamo Januari 2021.

Katika kitabu hicho, ilibainika Trump, 78 alimtumia Putin, 72 vifaa vya kujipima corona wakati ambapo virusi hivyo vilikuwa vikienea na kusababisha mauti ya raia duniani mnamo 2020.

Ufichuzi huo unazua wasiwasi iwapo Urusi huenda ikaingilia kura za Amerika ambazo zitapigwa mnamo Novemba 5 na kumsaidia Trump kupata ushindi.

Trump anawania kupitia chama cha Republican huku makamu wa Rais Kamala Harris akimenyana naye kupitia Democrats. Harris hasa amekuwa akimshambulia kuhusu madai ya kumtumia Putin vipimo vya virusi vya corona.

Katika kitabu hicho, Woodwad anasema Trump na Putin walizungumza pia mwaka huu. Trump aliamrisha mmoja wa walinzi wake aondoke afisini mwake jumba la Mar-a-Lago ili apige simu na kuzungumza na kiongozi huyo wa Urusi.

Hata hivyo, kikosi cha kampeni cha Trump kimepuuza madai hayo. Steven Cheung, aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano wa kiongozi huyo alisema kilichoandikwa katika kitabu hicho ni uongo.

Trump mwenyewe pia alikanusha madai hayo akisema Woodward ni msimulizi mbaya wa hadithi anayejikita katika kuandika uongo kumchafulia jina wakati ambapo kampeni nazo zimenoga.

Mnamo Jumatano, serikali ya Urusi pia ilipuuza madai kuwa Putin amekuwa akiwasiliana na rais huyo wa zamani wa Amerika.
“Huo ni uongo,” akasema Msemaji wa Ikulu Dmitry Peskov.

Hii si mara ya kwanza ambapo Woodward analenga kiongozi wa Amerika. Mwanahabari huyo anafahamika sana kwa kuandaa uchunguzi ambao ulichangia kuporomoka kwa utawala wa Rais Richard Nixon mnamo 1974.

Kitabu chache kimeonekana kufufua madai kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa Amerika mnamo 2016 na kumsaidia Trump kumbwaga aliyekuwa mwaniaji wa Democrats Hillary Clinton.

Uhusiano wa karibu kati ya Trump na Putin pia umeonekana kwenye vita kati ya Urusi na Ukraine. Huku utawala wa Rais Joe Biden ukiegemea upande wa Ukraine, Trump ameonekana kuunga Urusi kwenye vita hivyo japo hajasema hilo waziwazi.

Wakati wa mahojiano mwezi uliopita, Trump alikataa kujibu swali iwapo angependelea Ukraine ishinde vita hivyo. Alisema tu kuwa akichukua madarakani vita hivyo vitasitishwa ila hakusema mbinu atakayotumia.

Mnamo Septemba mwezi uliopita, Trump alikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky Marekani ambako alimtaka kiongozi huyo asitishe msimamo mkali na akubali kuongea na Putin ili vita kati ya mataifa hayo mawili vikomeshwe.