Kimataifa

Idadi ya waliokufa kwenye maporomoko Uganda yapanda hadi 17

Na REUTERS December 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

IDADI ya watu waliokufa kutokana na maroporomoko ya ardhi mashariki mwa Uganda imeongezeka hadi 17. Kufikia sasa, watu 100 hawajulikani waliko, kulingana na msemaji mmoja wa serikali.

Maporomoko hayo yalitokea Jumatano, kufuatia mvua kubwa iliyoshuhudiwa katika Wilaya ya Bulambuli lililoko umbali wa kilomita 300 kutoka jiji la Kampala na kufunika nyumba kadhaa.

Picha za televisheni zilionyesha eneo kubwa lililofunikwa na matope. Sehemu zilizofunikwa zilikuwa na makazi na shule hapo awali.

Manusura walilia kwa sauti za juu kwa kukosa wapendwa wao huku wahudumu wa mashirika ya uokoaji wakichimbua matope kusaka manusura zaidi.

Charles Odongtho, ambaye ni msemaji wa Afisi ya Waziri Mkuu, alisema awali serikali ilikuwa imewaonya watu wanaoishi katika maeneo hatari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa janga kama hilo msimu wa mvua utakapoanza.

Aliambia shirika la habari la Reuters kwamba alishtushwa na idadi ya watu waliokufa ikizingatiwa asasi husika za serikali zilitoa onyo la mapema.

Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda, angalau nyumba 45 zilifunikwa kabisa na matope huku nyumba nyingine zikiharibika.

Ignatius Wamakuyu Mudimi, ambaye ni mbunge katika Kaunti ya Elgon, alisema mpwa wake ambaye juzi alijifungua ni miongoni mwa watu waliokufa.

“Alizikwa kwenye matope pamoja na mwanawe mchanga,” alisema kwenye mahojiano na runinga ya NTV, Uganda.

Nchi ya Uganda imeshuhudia mvua kubwa tangu Oktoba mwaka huu na hivyo kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo.

Mnamo Jumanne, mvua kubwa ilisababisha Mto Nile, unaopitia Uganda, kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika barabara kuu inayoeleka kaskazini mwa nchi hiyo, kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Barabara (UNRA) na polisi.

Imetfasiriwa na Charles Wasonga