Ipswich Town waonja ushindi EPL baada ya miaka 22, Man U wakifufuka kabisa
LONDON, Uingereza
IPSWICH Town, ambao wamerejea Ligi Kuu ya Uingereza baada ya misimu 20, wameonja ushindi wa kwanza katika ligi hiyo kwa kuduwaza wenyeji wao Tottenham Hotspur 2-1 mjini London, Jumapili.
Tractor Boys wanavyofahamika kwa jina la utani, wamelima Spurs kupitia mabao ya kiungo Sammie Szmodics na mvamizi matata Liam Delap yaliyopatikana dakika ya 31 na 43. Delap alichangia katika kuzalishwa kwa magoli yote mawili.
Mshambulizi wa Suprs, Dominic Solanke alipoteza nafasi ya wazi ya kusawazisha 2-2 katika dakika za lala-salama. Solanke pia alinyimwa bao la VAR dakika ya 49 kabla ya Rodrigo Bentancur kufungia Spurs bao la kufutia machozi dakika ya 69.
Ni ushindi wa kwanza wa Ipswich kwenye EPL katika kipindi cha miaka 22, lakini wa nne mfululizo dhidi ya Spurs baada ya kuwanyuka 3-0 (Desemba 30, 2000), 2-1 (Desemba 22, 2001) na 2-1 (Januari 12, 2002).
Kabla ya ushindi mbichi Jumapili, Ipswich walikuwa wamepoteza mechi tano mfululizo dhidi ya timu kutoka London. Tottenham walitawala karibu kila idara ikiwemo umilikaji wa mpira 66-34, makombora 17-8 na kona 12-2, lakini mwisho wa siku Ipswich ndiyo ilitia kapuni alama tatu.
Ushindi unapaisha Ipswich kutoka nafasi ya 19 hadi 17 kwenye ligi hiyo ya klabu 20. Spurs wanasalia nafasi ya 10 kwa alama 16. Ipswich wamezoa alama nane.
Katika mechi nyingine zimesakatwa Jumapili, Nottingham Forest wamefyekwa 3-1 na Newcastle kupitia mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Alexander Isak, Joelinton na Harvey Barnes.
Murillo aliweka Forest 1-0 juu dakika ya 21 kabla ya Newcastle kujitokeza kivingine katika kipindi cha pili. Nao Manchester United wamepepeta Leicester 3-0 kupitia mabao ya Bruno Fernandes, Victor Kristiansen (alijifunga) na Alejandro Garnacho ugani Old Trafford.