Jeshi la Sudan latwaa Ikulu mapambano dhidi ya RSF yakiendelea
KHARTOUM, SUDAN
JESHI la Sudan Ijumaa (Machi 21, 2025) lilitwaa usukani wa Ikulu, hii ikiwa hatua kubwa kwenye vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kati yake na wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF).
Jeshi lilitwaa Ikulu ya Rais baada ya kuendesha oparesheni kali ya kuwanasa wanachama wa RSF.
Milio ya risasi iliskika kila mahali jijini Khartoum makabiliano kati ya mirengo hiyo miwili yalipokuwa yakiendelea.
Mnamo Aprili 2023, RSF ilitwaa usimamizi wa Ikulu pamoja na baadhi ya maeneo ya jiji la Khartoum, lakini jeshi limekuwa likipiga hatua na kutwaa baadhi ya maeneo ambayo walikuwa wamepoteza kwa wapiganiaji hao.
Bado RSF inadhibiti baadhi ya maeneo jijini Khartoum na jiji la Omdurman pamoja na magharibi mwa Sudan.
RSF imekuwa ikipambana sana kutwaa eneo la Darfur ambalo limeshuhudia machafuko zaidi kutoka kwa jeshi.
Kutwaa Ikulu ya rais kumefasiriwa kuwa kutaharakisha jeshi kupata Sudan ya Kati, huku pande zote mbili zikionekana kudhibiti mashariki na magharibi mwa taifa hilo.
Juhudi zozote za amani zimepuuzwa na jeshi na RSF.
Vita hivyo vilizuka baada ya pande zote mbili kutofautiana kuhusu upokezanaji wa mamlaka kwa raia.
Machafuko kati ya RSF na UN yamesababisha janga kubwa la kibinadamu, huku Umoja wa Kimataifa ukisema yameeneza magonjwa na njaa katika maeneo tofauti ya taifa hilo.
RSF na jeshi, zote zimekashifiwa kwa kusababisha uhalifu wa kivita huku RSF ikishutumiwa kwa mauaji ya halaiki lakini imekanusha hilo.