Kimataifa

Kamala Harris aingia sokoni kutafuta mgombea mwenza baada ya Biden kumwachia tiketi

Na MASHIRIKA July 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WASHINGTON, AMERIKA

MAKAMU wa Rais wa Amerika, Kamala Harris anapojiandaa kwa uteuzi rasmi kama mgombeaji wa urais wa chama cha Democratic ili apambane na Donald Trump wa Republican, suala la ni nani atakuwa mwaniaji mwenza wake limeanza kuangaziwa.

Atahitajika kuteua mwaniaji mwenza kabla ya wajumbe wa chama hicho tawala kupiga kura mwezi ujao katika kongamano litakalofanyika Chicago kuidhinisha rasmi mgombeaji wake wa urais.

Imeripotiwa kuwa kundi maalum limeteuliwa kuwapiga msasa watu kadhaa ili kubaini atakayefaa zaidi kushirikiana na Harris kukiwezesha chama hicho kushinda urais katika uchaguzi wa Novemba 5, 2024.

Kihistoria, nchini Amerika na mataifa mengine, makamu wa rais huteuliwa kuboresha nafasi ya mgombeaji wa urais kushinda.

Kwa hivyo, waratibu wa mikakati wa Democrat wanaamini Harris, ambaye ni Mwamerika Mweusi, atateua mwanaume Mwamerika Mweupe kutoka moja ya majimbo muhimu katika kuamua mshindi wa urais.

Watu wafuatao wametajwa kama ambao wanaweza kuchukua nafasi ya mgombeaji mwenza wa Harris.

Josh Shapiro, Gavana wa Pennsylvania: Shapiro amewavutia wengi tangu alipochaguliwa mnamo 2022 katika jimbo hilo ambalo Trump alishinda katika uchaguzi wa urais wa 2016.

Gavana huyo, aliyehudumu hapo awali kama mwanasheria mkuu katika jimbo hilo, amehudumia chama cha Democrat katika nyadhifa mbalimbali.

Andy Beshear, Gavana wa Kentucky: Beshear amejijengea sifa kama gavana aliyeandikisha ufanisi mkubwa katika jimbo hilo lenye idadi kubwa la wafuasi wa chama cha Republican.

Akiwa na umri wa miaka 46, Beshear ni kati ya magavana wenye umri mdogo zaidi Amerika.

Wengine wanaopigiwa upatu kuteuliwa kuwa mgombeaji mwenza wa Harris ni pamoja Seneta wa Arizona Mark Kelly, Gavana wa jimbo la North Carolina Roy Cooper, Gavana wa Illinois JB Pritzker, na Gavana wa California Gavin Newsom, miongoni mwa wengine.

Tangu Rais Joe Biden ajiondoe kwenye kivumbi cha urais wa Novemba, hakuna aliyejitokeza kumpinga Kamala kumrithi mkubwa wake.

Hadi kufikia Jumanne, wajumbe wengi walikuwa wamemuunga mkono kuchukua tiketi ya urais.