Kiongozi wa Kundi la wapiganaji Hamas auawa
KIONGOZI wa kundi na wapiganaji la Hamas, Ismail Haniyeh, ameuawa nchini Iran, kundi hilo la wanamgambo wa Palestina lilisema Jumatano, Julai 31, 2024 na kutaja shambulio hilo kama “ongezeko kali la mapigano” ambalo halitaafikia malengo yake.
Kikosi cha Revolutionary Guards cha Iran kilithibitisha kifo cha Haniyeh, saa chache baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo, na kusema kuwa kinafanya uchunguzi.
Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa mamlaka ya Israeli.
Ikulu ya White House, Amerika haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu kuuawa kwa Haniyeh.
Habari hizo, ambazo zilijiri chini ya saa 24 baada ya Israeli kudai kumuua kamanda wa Hezbollah ambaye ilisema ndiye aliyehusika na shambulio baya katika milima ya Golan inayokaliwa na Israeli, zinaonekana kurudisha nyuma uwezekano wa makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza.
“Mauaji haya yaliyofanywa na Israel kwa ndugu Haniyeh, ni ongezeko kubwa la mapigano ambalo linalenga kuvunja moyo Hamas,” afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri aliambia Reuters.
Alisema Hamas itaendelea na njia iliyokuwa ikifuata, na kuongeza: “Tuna uhakika tutaibuka na ushindi.”
Haniyeh, ambaye kwa kawaida anaishi Qatar, amekuwa akihusika na diplomasia kimataifa katika kundi hilo la Palestina huku vita vilivyoanzishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 vikipamba huko Gaza, ambapo wanawe watatu waliuawa katika shambulio la angani lililotekelezwa Israel.
Akishikilia wadhifa wa juu katika Hamas alioteuliwa mwaka 2017, Haniyeh amekuwa akihamia kati ya Uturuki na mji mkuu wa Qatar Doha, akikwepa njia za usafiri za Ukanda wa Gaza uliozingirwa na kumwezesha kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano au kuzungumza na mshirika wa Hamas, Iran.