Magufuli aahidi uchaguzi huru kampeni zikitamatika leo
Na Mwandishi Wetu
KAMPENI za Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania zinaisha saa kumi na mbili jioni leo huku Watanzania wakijiandaa kuchagua rais, wabunge na madiwani kesho.
Rais John Pombe Magufuli atamalizia kampeni zake jijini Dodoma huku mshindani wake wa karibu Tundu Lissu akiandaa mkutano wake wa mwisho jijini Dar es Salaam.
Jana, Chama Cha Mapinduzi (CCM) chake Rais Magufuli kilishikilia kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakiongozwa na rais mstaafu wa Burundi, Sylevestre Ntibantunganya, walikutana na viongozi wa CCM na Chadema ambapo walihakikishiwa kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki.
Rais Magufuli anategemea miradi yake ya maendeleo aliyoitekeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kushawishi Watanzania kumchagua tena.
Katika kampeni zake, Rais Magufuli amekuwa akiorodhesha miradi mbalimbali ambayo ametekeleza kama vile usambazaji wa umeme vijijini, ufufuzi wa shirika la safari za ndege, utengenezaji wa meli, elimu ya bure, ujenzi wa barabara na treni ya kisasa (SGR) kati ya mingineyo.
Rais Magufuli amekuwa akisema kwamba amefanikiwa kutoa elimu bila malipo katika ngazi ya shule za msingi na sekondari na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi wa sekondari kutoka milioni 1.6 mwaka 2015 hadi milioni 2.2 mwaka jana.
Rais Magufuli pia anasema wakati wa utawala wake amefanikiwa kuongeza vituo vya afya kutoka 7,014 mwaka 2015 hadi 8,446 mwaka huu.
Katika ilani ya CCM ya 2020 – 2025 yenye kurasa 308, Rais Magufuli ameahidi kuongeza nafasi za ajira, kuboresha uchumi, kuimarisha sekta ya kilimo, kukatisha fedha haramu zinazotokana na dawa za kulevya na utengenezaji na usambazaji wa fedha bandia.
Katika kampeni zake za jana, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kudumisha amani.
Kwa upande mwingine, Bw Lissu amekuwa akiwashawishi Watanzania kumchagua huku akisema kuwa atafutilia mbali baadhi ya ushuru; ahadi ambayo imepuuziliwa mbali na viongozi wa CCM kuwa nchi haiwezi kuendeshwa bila ushuru.
Lissu pia anasema kuwa Rais Magufuli amejikita katika kuboresha miundomsingi kama vile kununua ndege, kujenga reli na barabara huku Watanzania wakiendelea kuzama kwenye umaskini.
Kulingana na Lissu, Rais Magufuli amekuwa akiendesha Tanzania kidikteta hivyo Watanzania wanahitaji kuwa huru kwa kumchagua kesho.
Katika uchaguzi mkuu wa 2015, Rais Magufuli alishinda kwa asilimia 58 huku Edward Lowassa wa Chadema akipata asilimia 40.