Majaji wakuu Afrika Mashariki waungana kuimarisha haki
Na BENSON MATHEKA
MAJAJI wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekubali kushirikiana ili kuimarisha mfumo wa utoaji haki katika nchi zao na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Kwenye taarifa ya pamoja waliyotoa baada ya kukutana katika hoteli moja jijini Nairobi, majaji hao walitambua umuhimu wa teknolojia na maadili miongoni mwa nguzo za kuimarisha mfumo wa haki katika eneo la Afrika Mashariki.
“Tumekubaliana kushirikiana katika kutambua, kutekeleza na kubadilisha maoni kuhusu mbinu za ubunifu katika kuimarisha utoaji wa haki ikiwa ni pamoja na kukumbatia teknolojia na kuweka mikakati ya kuimarisha maadili,” walisema majaji hao.
Kwa pamoja, walikubali kuwa mrundiko wa kesi katika korti za eneo la Afrika Mashariki ni kizingiti katika utoaji wa haki na wakajitolea kutafuta mbinu za kuhakikisha kesi hazichukui muda mrefu mahakamani kabla ya kuamuliwa.
“Tunatambua uwepo wa mrundiko wa kesi na athari zake kwa utoaji wa haki na tumejitolea kutafuta mbinu za kumaliza mrundiko huo katika mahakama zote Afrika Mashariki,” ilisema taarifa ya pamoja ya majaji hao.
Kuhusu suala la rushwa katika mahakama, walisema kwamba wataimarisha mifumo ya uwazi kwa maafisa wa mahakama na kurahisisha mawasiliano na umma.
Hata hivyo, walisema kwamba ili kufaulu ni lazima idara ya Mahakama katika kila nchi itengewe pesa za kutosha kufanikisha miradi na malengo yake.
“Japo tunatambua na kuelewa kwamba mapato ya nchi zetu ni ya chini, pesa zinazotengewa idara za mahakama kwa sasa ni haba sana kuliko mahitaji ya mahakama ya kutoa huduma za kiwango cha juu za haki kwa raia. Tumekubaliana kwamba tutaendelea kuzungumza na mabunge na serikali kuu kuongeza pesa zinazotengewa mahakama,” walisema.
Majaji wakuu hao ni David Kenani Maraga wa Kenya aliyekuwa mwenyeji wa mkutano huo, Sam Rugege wa Rwanda, Bart Katureebe wa Uganda, Ibrahim Hamisi Juma wa Tanzania, Chan Madut wa Sudan Kusini, Omar Makungu wa Zanzibar na Dkt Emmanuel Ugarishebuja wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Jaji Mkuu wa Somalia, Ibrahimu Sulaiman alihudhuria kama mwangalizi.