Kimataifa

VITUKO UGHAIBUNI: Mtoto wa miujiza azaliwa katika kisiwa ambapo kupata mimba ni marufuku

May 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

AFP na VALENTINE OBARA

RIO DE JANEIRO, BRAZIL

KISIWA kilicho Brazil kimepata mtoto wa kwanza baada ya miaka 12, kwani kuna marufuku dhidi ya wanawake kuzaa katika eneo hilo.

Mwanamke anayeishi katika kisiwa hicho cha Fernando de Noronha alikiuka sheria za kutozaa akajifungua Jumamosi iliyopita.

“Mama huyo ambaye hangependa kutajwa, alijifungua nyumbani kwake. Familia yake inasema hawakujua alikuwa mja mzito,” wasimamizi wa kisiwa hicho walisema kwenye taarifa iliyochapishwa na gazeti la O Globo.

Kisiwa hicho kidogo kina umaarufu wa kuhifadhi wanyamapori na kina watu karibu 3,000 pekee. Kulingana na mashirika ya habari, uzaaji ulipigwa marufuku kwa sababu hakuna chumba cha kujifungua hospitalini.

Kina mama waja wazito huhitajika kusafiri karibu kilomita 365 kuvuka bahari hadi mji wa karibu ambao ni Natal.

Mama huyo ambaye ana mtoto mwingine aliyezaliwa katika nchi kavu, alinukuliwa kusema hakuhisi chochote alipokuwa mja mzito.

“Ijumaa usiki nilihisi uchungu na nilipoenda msalani niliona kitu kikitoka katikati ya miguu yangu. Hapo ndipo baba mtoto alikuja na kukichukua. Kilikuwa ni kitoto, msichana. Nilipigwa na butwa,” akasema.