• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mwanamke kulipwa Sh61m kwa kulazimishwa kujifungua akiwa na pingu

Mwanamke kulipwa Sh61m kwa kulazimishwa kujifungua akiwa na pingu

MASHIRIKA Na PETER MBURU

SERIKALI ya jimbo la New York, Amerika itamlipa mwanamke Sh61 milioni, baada ya kulazimishwa kujifungua akiwa na pingu Februari 2018.

Katika kesi aliyowasilisha mahakamani, Jane Doe alisema alipatwa na uchungu wa kuzaa saa chache baada ya kukamatwa na polisi Februari 7, 2018, lakini akalazimishwa kujifungua akiwa amefungwa pingu, siku iliyofuata.

Hii ilikuwa licha ya kuwa kumtia pingu mwanamke mja mzito ni hatia jimbo la New York, kulingana na sheria iliyoundwa 2009, na kuratibiwa 2015 kwa kuharamisha matumizi ya nguvu dhidi ya mwanamke mja mzito.

Alipopatwa na uchungu zaidi, alipelekwa hospitalini Februari 8, akiwa amefungwa pingu mikononi na minyororo miguuni, hivi kwamba hakuwa akiweza kuipanua.

Kulingana na Doe, madaktari waliwataka maafisa waliokuwa naye kumfungua pingu na minyororo hiyo kwa kuwa ilihatarisha maisha yake na ya mtoto. Hata hivyo, polisi hao wanaripotiwa kujibu kuwa kwa mujibu wa sheria za polisi wa New York, alifaa kukaa hivyo.

“Bi Doe hakujaribu kubishana nao ama kuonyesha tabia yoyote ya kuwafanya polisi kumfunga hivyo. Alikuwa ameshtuka kwa ajili yake na mtoto wake,” malalamishi yake kortini yakasema.

Wakati madaktari walilalamika zaidi ndipo polisi hao walimfungua minyororo miguuni, dakika chache kabla yake kujifungua, kisha wakamfunga tena baada ya kumaliza kujifungua.

Alilazimika kumlisha mtoto kwa mkono mmoja, huku akirejeshwa jela akiwa na pingu.

Kulingana na Doe, matukio hayo yalimwathiri kisaikolojia na amekuwa akikumbwa na ndoto mbaya mara kwa mara, kando na kushtuka kila wakati.

Baada ya kusikiza malamishi yake, korti iliamua Doe alipwe Sh61 milioni kutokana na jinsi haki zake zilivunjwa wakati huo, amri ambayo serikali ya New York imetii na kuahidi kumlipa.

You can share this post!

Kuria akataa marupurupu, aamuru pesa hizo zipelekwe...

Punda aundiwa miwani baada ya kuumia jicho

adminleo