Mwanamume anaswa na bunduki mkutano wa Trump katika ‘jaribio lingine la mauaji’
CALIFORNIA, AMERIKA
MWANAMUME aliyekamatwa katika kituo cha ukaguzi karibu na mahala pa mkutano wa mgombea urais wa Republican Donald Trump jimboni California alishtakiwa baada ya kupatikana na bunduki yenye risasi, polisi walisema.
Aidha, mshukiwa huyo alipatikana na paspoti kadhaa bandia na nambari za usajili wa magari.
Msimamizi Mkuu wa Kaunti ya Riverside, Chad Bianco, alisema aliamini kuwa idara yake ilizima jaribio la mauaji.
Mshukiwa aliachiliwa huru kwa dhamana mnamo Jumamosi jioni, kulingana na rekodi za gereza.
Afisa mmoja wa utawala wa jimbo hilo Jumapili alisema kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo.
“Kile tunachofahamu ni kuwa alikuwa na paspoti yenye majina tofauti, alikuwa na gari lenye nambari feki ya usajili na bunduki zenye risasi,” Bianco akasema kwenye kikao na wanahabari Jumapili jioni.
“Ama kwa kweli inaaminika kuwa tulitibua jaribio jingine la mauaji,” akaeleza.
Mshukiwa huyo, mwanamume mwenye umri wa miaka 49, aliyetambuliwa kama Vem Miller ni mkazi wa Las Vegas.
Alisimamishwa na maafisa wawili wa usalama Jumamosi na kusukumwa kuzuizini, kulingana na afisi ya msimamizi mkuu wa kaunti hiyo.
Wakati huo, Trump hakuwa amepanda jukwaani.
Rekodi za gereza zinaonyesha kuwa Miller aliachiliwa huru kwa dhamana ya dola 5,000 (Sh750,000) Jumamosi jioni baada ya kushtakiwa kwa kosa la kuwa na bunduki yenye risasi bila kibali maalumu.
Juhudi za kumfikia mshukiwa huyo ili ahojiwe hazikufaulu Jumapili.
“Kisa hicho hakikuwa na athari zozote za kiusalama kwa Rais wa zamani Trump au waliohudhuria mkutano huo,” afisa ya msimamizi wa kaunti ya Riverside alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Amerika iliyoko kati mji wa Los Angeles, kwenye taarifa katika tovuti yake pia ilisema kuwa Trump hakuwa hatarini.
Taarifa hiyo ilinukuu duru za Idara ya Usalama Nchini Amerika.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa japo watu wengi hawajakamatwa kuhusiana na kisa hicho, uchunguzi ulikuwa ukiendelea.
Mnamo Julai mwaka huu, Trump aliponea kifo kwa tundu la sindano baada ya kujeruhiwa sikioni na risasi iliyofyatuliwa na mshambuliaji mmoja alipokuwa katika mkutano wa kampeni mjini Butler, jimbo la Pennsylvania.
Mnamo Septemba, mwanamume mwingine alifunguliwa mashtaka kwa kujaribu kumuua Trump.
Hii ni baada ya maafisa wa idara ya usalama wa rais kumpata na bunduki akiwa amejificha karibu na uwanja mmoja wa gofu unaotumiwa na Trump. Mwanamume huyo alikana mashtaka hayo.
Majaribio hayo ya mauaji ya Trump yameibua maswali kuhusu utendakazi wa maafisa wa idara maalumu ya kutoa usalama kwa rais na wagombeaji urais.
Wakati uo huo, umaarufu wa Makamu wa Rais Kamala Harris unaonekana kupungua huku ule wa Trump ukiimarika, chini ya mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa urais kufanyika Novemba 5 mwaka huu.
Matokeo ya kura ya maoni yaliyoendeshwa na mashirika matatu yanaonyesha kuwa pengo kati ya umaarufu wa Harris na Trump unapungua au umezibwa kabisa.
Kwa mfano matokeo ya kura ya maoni yaliyoendeshwa na shirika la NBC News yanaonyesha kuwa wagombeaji hao wa vyama vya Democrat na Republican wanatoshana kwa umaarufu wa asilimia 48.
Kwa upande mwingine matokeo ya kura ya maoni yaliyoendeshwa na la ABC News/Ipsos yanaonyesha kuwa Harris anaongoza kwa asilimia 50 huku Trump akiwa na umaarufu wa asilimia 48.
Kulingana na matokeo ya mwezi jana, Harris alikuwa anaongoza kwa asilimia 50 huku Trump akiwa na umaarufu wa asilimia 48.