Mzozo: Mali yakatiza uhusiano wake na Ukraine
MALI imekatiza uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine, baada ya afisa mmoja wa cheo cha juu Ukraine kukubali kuwa nchi hiyo ilisaidia katika mauaji ya mamluki wa Wagner kutoka Urusi na wanajeshi wa Mali Julai 2024.
Waasi wanaojulikana kama, Northern Tuareg, wanasema waliua mamluki 84 wa Wagner na wanajeshi 47 wa Mali katika mapigano yaliyodumu kwa siku tatu Julai 2024.
Hiyo ilionekana kuwa tukio kubwa la kulemewa kwa mamluki hao kutoka Urusi tangu walipoingilia vita nchini Mali miaka miwili iliyopita.
Mnamo Julai 29, msemaji wa Shirika la Ujasusi la Jeshi la Ukraine (GUR) Andriy Yusov aliambia shirika la habari nchini humo Suspilne kuwa waasi wa Mali walipokea “maelezo yote waliyohitaji, yaliyowasaidia kuendesha operesheni dhidi ya wahalifu wa kivita kutoka Urusi”.
Utawala wa Mali ulisema ulipokea “kwa mshangao” kauli ya Yusov kwamba Ukraine ilihusika katika shambulio lililotekelezwa na makundi ya kigaidi yaliyopelekea vifo vya maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Mali.
Msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga alisema kutokana na shambulio hilo “tunakatiza uhusiano na Ukraine mara moja.”
Aidha, Mali ilisema hatua hiyo pia imechangiwa na kauli iliyotolewa na Balozi wa Ukraine nchini Senegal Yurii Pyvovarov kwamba nchi yake “ilitoa usaidizi uliochangia shambulio la kigaidi” Mali.
Pyvovarov alisema hayo kwenye video aliyoweka katika mtandao wa kijamii wa Facebook, hali iliyokasirisha serikali ya Senegal.
Kulingana na Kanali Maiga, hatua ya Ukraine iliingilia uhuru wa Mali na inaonekana kama uchokozi usiokubalika na uungwaji mkono wa ugaidi wa kimataifa.
Wiki jana, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Urusi Sergey Lavrov alizungumza na mwenzake wa Mali Abdoulaye Diop kwa njia ya simu akikariri kujitolea kwa nchi yake kuisaidia Mali.
Jeshi la Mali lilitwaa mamlaka katika mapinduzi ya 2020 na wamejitolea kukomboa taifa hilo kutoka kwa udhibiti wa makundi na waasi yenye uhusiano na makundi ya kigaidi ya Al-Qaeda na ISIL.
Wanajeshi hao wamebuni uhusiano mwema na Urusi na mamluki wa Wagner wamekuwa wakiendesha shughuli za kuleta amani nchini Mali tangu mwishoni mwa 2021. Mamluki hao walichukua nafadi ya wanajeshi wa Ufaransa na vikosi vingine vya walinda usalama wa kimataifa.