Nigeria yaanza kusaka wasichana 110 waliotekwa na Boko Haram
Na AFP
ABUJA, Nigeria
SERIKALI ya Nigeria imeanza harakati za kuwatafuta wasichana 110 wa shule moja, wanaoaminika kutekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram wiki iliyopita.
Serikali ilisema imetuma wanajeshi zaidi na ndege ili kuimarisha operesheni hiyo.
Wasichana hao walitoweka muda mfupi baada ya wanamgambo hao kuvamia shule yao Jumatatu iliyopita katika mji wa Dapchi, jimbo la Yobe.
Rais Muhammadu Buhari alitaja kisa hicho kama “janga la kitaifa” huku akiomba msamaha kwa familia za wasichana hao. Tukio hilo linajiri baada ya jingine lililofanyika mnamo 2014, ambapo wasichana 276 walitekwa nyara na kundi hilo.
Familia za wasichana hao zimekumbwa na ghadhabu, baada ya ripoti kuibuka kwamba serikali ilikuwa imewaondoa wanajeshi wake katika maeneo muhimu ya Dapchi, mwezi uliopita. Mji huo uko umbali wa kilomita 275 kutoka eneo la Chibok, ambako shambulio la 2014 lilifanyika.
Wanamgambo hao wanadaiwa kuvamia Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi ya Serikali, ambayo huwa na wasichana pekee.
Wakazi walio karibu walisema kuwa vikosi vya kijeshi vilijibu shambulio hilo mara moja kwa kutumia ndege za kivita.
Awali, mamlaka zilikanusha kwamba wasichana hao walikuwa wametekwa nyara, zikishikilia kuwa walikuwa wamejificha ili kutoonekana na washambuliaji hao.
Kundi la Boko Haram limekuwa likipigania kubuniwa kwa taifa huru katika ukanda wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hadi sasa, wasichana waliotekwa nyara awali wangali kufahamika waliko.
Serikali baadaye ilitoa taarifa ikithibitisha kutekwa nyara kwa wanafunzi hao.
Uvamizi shuleni
“Serikali ya Nigeria ingependa kuthibitisha kwamba wanafunzi 110 kutoka Tasisi ya Kiufundi ya Serikali, mjini Dapchi hawajulikani waliko baada ya wanamgambo wa Boko Haram kuvamia shule yao,” ilisema taarifa kutoka Wizara ya Habari na Mawasiliano.
Kisa hicho kimeibua maswali kuhusu hali ya utayarifu wa jeshi hilo kuwakabili wanamgambo hao. Aidha, hili linajiri baada jeshi hilo kudai kwamba lilikuwa tayari kuwazima wanamgambo hao.
Kauli ya Rais Buhari pia imekosolewa vikali na baadhi ya wanaharakati, huku wakiamini kwamba serikali imeshindwa kabisa kulikabili kundi hilo.
Alipochaguliwa kama rais mnamo 2015, Bw Buhari, ambaye alikuwa mtawala wa kijeshi aliahidi kukabiliana na kundi hilo. Hii ni baada ya mtangulizi wake, Goodluck Jonathan kulaumiwa vikali kwa kushindwa kulikabili.
Mwalimu mmoja katika taasisi hiyo, Amsani Alilawan, alisema kwamba kulikuwa na wanajeshi katika eneo hilo hadi mwezi uliopita, ila wakaondolewa.
“Waliwaondoa wanajeshi hao wote na kuwahamisha katika maeneo mengine,” akasema.