Rais Biden akana kuita wafuasi wa Trump ‘takataka’ kwenye kampeni
RAIS wa Amerika, Joe Biden, Jumanne alilazimika kutoa ufafanuzi kuhusu matamshi yake baada ya kudaiwa kuwarejelea wafuasi wa mwaniaji wa Urais wa Republican Donald Trump kama ‘takataka’.
Akiongea mnamo Jumanne, Biden alijitetea kuwa hakutoa matamshi kama hayo akisema maneno yake yalifasiriwa vibaya na upande wa Trump.
Alisikitika kuwa wanachama wa Republican sasa wanatumia suala hilo kumrejelea kama mbaguzi wa rangi na kiongozi asiyethamini Waamerika.
“Siku ile nyingine, akihutubu katika mkutano wake, Biden alirejelea Puerto Rico kama kisiwa kinachoelea na takataka,” akasema mmoja wa wafuasi wa Trump akirejelea kisiwa hicho kama kilicho nadhifu na chenye watu wastaarabu.
“Takataka ninayojua inaelea hapo nje ni wafuasi wake, chuki zake na kuwadhihaki Waamerika weusi,” akaongeza.
Ni kauli hii ndiyo imemchongea Biden na kuwakasirisha wafuasi wa Trump waliodai walidunishwa.
Baadhi ya wafuasi wa Trump walihusisha kauli hiyo na ile aliyoitoa Hillary Clinton mnamo 2016 ambapo aliwarejelea wakazi wa Puerto Rico kama watu waliokuwa wakiishi maisha ya dhiki na katika hali mbaya.
Msemaji wa White House, Andrew Bates, alipuuza madai kuwa Biden alikuwa akiwarejelea wafuasi wa Trump. Bates alisema Rais Biden alikuwa akirejelea matamshi ya chuki ambayo yalitolewa katika mkutano wa Trump katika Bustani ya Madison Square. Kwenye mtandao wake wa ‘X’, Biden alijitetea kuhusu suala hilo.
“Mapema leo nilirejelea matamshi ya chuki yaliyotolewa na mfuasi wa Trump kuhusu Puerto Rico kwenye mkutano aliouandaaa katika Bustani ya Madison kama takataka. Hilo ndilo neno nililofikiria nilitumie kumrejelea.
“Hatua ya Trump kuwakashifu na kuwadhihaki Waamerika wenye asili ya Kilatino hayafai kabisa. Matamshi yaliyotolewa kwenye mkutano wa Trump hayasawiri jinsi tulivyo kama taifa,” akaandika Biden.
Kwa wafuasi wa Democrat, baadhi wanahisi Biden angechunga ulimi wake na akome kuyatoa matamshi yanayoweza kuharibu kura za makamu wake Kamala Harris wakati huu kampeni hizo zinapoelekea mkondo wa lala salama.
Biden, 81, alilemewa kwenye mjadala kati yake na Trump mnamo Juni kutokana na ukongwe wake na hilo ndilo lilichangia ajiondoe kwenye kiny’ang’anyiro cha kusaka fursa ya kuchaguliwa tena kuhudumu kwa muhula wa pili wa miaka minne.
Hata ndani ya chama chake cha Democrat, baadhi ya viongozi walihoji kuhusu uwezekano wake wa kuongoza Amerika na nafasi yake ya kumshinda Trump iwapo angewania tena urais mwaka huu.
Tangu Biden ajiondoe, Harris amekuwa akiendeleza kampeni kali ya kutwaa uongozi wa nchi wakati uo huo akitetea uongozi wa Biden. Harris, 59, mwenyewe amekuwa akijisawiri kama kiongozi ambaye atapisha uongozi wa kizazi kipya.
Zimesalia siku tano pekee kwa uchaguzi mkuu wa Amerika kufanyika na kuna ushindani mkali kati ya Trump na Harris; kura za maoni zikionyesha umaarufu wao unatenganishwa na asilimia moja pekee.
Wawili hao wanatarajiwa kuelekeza juhudi zao katika kutwaa kura za majimbo saba ambazo zitaamua mshindi wa kura hiyo ya Novemba 5.