Kimataifa

Rais Museveni naye pia akataa kutia saini bajeti; airudisha bungeni

Na DAILY MONITOR June 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMPALA, UGANDA

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amekataa kutia saini Mswada wa Matumizi ya Pesa za Bajeti 2024 hadi Bunge la nchi hiyo litakaporejesha Sh750 bilioni zilizotengewa kwa ajili ya matumizi ya mipango muhimu ya serikali katika mwaka wa kifedha 2024/2025.

Museveni alifaa kutia saini mswada huo jana baada ya kukutana na Baraza la Mawaziri Ikuluni ambapo alisisitiza vita vyake dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya pesa za umma.

Msimamo huo mkali wa Rais Museveni unatishia utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa 2024/2025 na unaweka shughuli zilizopangwa kuwa hatarini kwa kuwa mwaka huu wa fedha utakamilika Jumapili, Juni 30.

Mswada wa matumizi ya pesa za bajeti ni sheria yenye kiasi cha fedha kitakachotumiwa na kila wizara ya serikali, idara na serikali za mitaa, na kuidhinisha utoaji wa fedha hizo kutoka kwa Mfuko Mkuu wa Hazina.

Lengo la Mswada huo lilikuwa kutoa idhini ya matumizi ya umma kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya USh30.314 trilioni ili kukidhi matumizi ya mwaka unaoishia Juni 30, 2025, na kuidhinisha mahitaji yaliyotolewa na Bunge.

Spika wa bunge hilo, Anita Among, aliripotiwa kuwa hakupokea stakabadhi zinazoonyesha kutoridhishwa kwa Rais Museveni.

Hata hivyo, ikitokea kwamba Rais atarejesha Mswada huo kwa ajili ya kuzingatiwa, Spika hatakuwa na jingine la kufanya ila kuurudisha Bungeni baada ya wabunge kutoka mapumzikoni.

Bunge, chini ya Ibara ya 79(1) ya Katiba, lina uwezo wa kutunga sheria kuhusu suala lolote la amani, utulivu, maendeleo na utawala bora wa Uganda.

Katiba inampa rais siku 30 kuidhinisha Mswada huo.

Hata hivyo, chini ya Kifungu cha 91(3) cha Katiba, Mswada unaweza kuwa sheria bila kibali cha rais iwapo ataurudisha Bungeni mara mbili.

Wakati baadhi ya wabunge wakimtuhumu Rais Museveni kwa kujaribu kunyakua mamlaka ya kisheria ya Bunge katika mchakato wa kupanga bajeti, wengine walizungumzia tatizo la muda mrefu ambalo linahitaji kuzingatiwa haraka, wakitaja matumizi mabaya ya mamlaka ya ugawaji na ushawishi katika kamati ya Bajeti.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wilfred Niwagaba alieleza:

“Bunge si taasisi ya mwisho na kwa kuzingatia Mswada huo, lina mamlaka ya kuuchunguza na kuufanyia marekebisho kama inavyofanya Miswada mingine,” alisema.

Aliongeza: “Kama Rais hataridhika, Ibara yote ya 91 ya Katiba ina maelezo ya kutosha kuhusu nini kitatokea, lakini hatimaye, Bunge lisipokubaliana na rais, basi litaangalia upya mswada huo na hatimaye kuwa sheria chini ya Kifungu cha 91(6) na (7) cha sheria.”

Mapema mwezi huu, Katibu Mkuu katika Wizara ya Fedha, Bw Ramathan Ggoobi, ambaye pia ni Katibu wa Hazina, aliwashutumu wabunge kwa kuvuruga Bajeti ya Kitaifa, kuhamisha na kuweka mahitaji yao katika maeneo bunge yao.