Kimataifa

Serikali ya DRC, waasi wa M23 walaumiana milipuko ikiua watu 13 na kujeruhi 68

Na REUTERS March 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINSHASA, DR CONGO

SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, Ijumaa zililaumiana kufuatia milipuko iliyotokea Alhamisi katika mkutano wa umma ulioitishwa na waasi hao mashariki mwa mji wa Bukavu iliyoua watu 13 na kujeruhi 68.

Majibizano hayo ya lawama yamezidisha taharuki eneo la mashariki mwa DR Congo ambako mji wa Bukavu unapatikana na ambao umeshuhudia vita baina ya M23 na jeshi la serikali.

Vita hivyo vimevuta mataifa jirani na kuibua taharuki ya kuzuka kwa vita vikubwa katika Ukanda wa Maziwa Makuu (Great Lakes Region).

Watu wakitoa damu katika Hospitali Kuu ya Bukavu ili ipewe raia waliojeruhiwa Alhamisi katika mkutano ulioitishwa na M23, mnamo Ijumaa. PICHA | REUTERS

Jeshi la DR Congo lilisema vikosi vya Rwanda – ambayo inaishutumu kwa kuunga mkono waasi wa M23 – vililipua roketi na guruneti katika mkutano huo wa umma katikati mwa Bukavu, uliokusanyika ili kusikiza hotuba ya mmoja wa viongozi wa waasi mnamo Alhamisi.

“Jeshi la Rwanda na mawakala wao walirusha vilipuzi na kufyatua risasi dhidi ya wananchi ambao, ingawa walilazimishwa kuhudhuria mkutano huo, walieleza kutofurahia vitendo vya Rwanda,” Wizara ya Usalama ya Congo ilisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X Ijumaa asubuhi.

Msemaji wa serikali ya Rwanda hakujibu ombi letu la kutaka kauli yao. Taifa hilo limekana mara kadha kwamba linaunga mkono M23.

Vifo, majeraha

Corneille Nangaa, ambaye ni kiongozi wa M23 na mratibu wa muungano wa makundi ya waasi (AFC) unaojumuisha M23, alinyooshea kidole cha lawama Rais Felix Tshisekedi kwa milipuko hiyo mjini Bukavu.

Aliambia kikao cha wanahabari Alhamisi kwamba guruneti zilizotupwa kwenye umati ndizo zile zinatumiwa na vikosi vya taifa jirani Burundi, ambavyo vinasaidia jeshi la DR Congo. Hatukuweza kudhibitisha madai hao kuhusu guruneti.

Msemaji wa jeshi la Burundi alisisitiza hakuna mwanajeshi wake yuko mjini Bukavu, lakini hakuzungumzia madai kuhusu guruneti.

Watu wawili walioshuhudia ghasia za Alhamisi walisema waliona mtu akijaribu kutupa guruneti dhidi ya msafara wa viongozi wa M23 lakini kilipuzi hicho kikaanguka kwa umati na kuua watu.

“Guruneti ililipuka haraka kabla hajairusha. Mlipuko ulimuua yeye pia.”

Nje ya hospitali kuu ya Bukavu duru za afya zilisema Alhamisi kwamba watu 68 walikuwa wakitibiwa majeraha.

Hata hivyo, hospitali hiyo ilisema haingetoa mwili wowote wa waliofariki dunia huku ikiagiza familia zilizokuwa zikisubiri maiti hizo ziache nambari za simu ili wahudumu wa afya wawasiliane nao baadaye.

Ijumaa takriban jamaa 30 za walioaga dunia walikuwa wakisubiri kutambua miili ya wapendwa wao nje ya mochari akiwemo Jean-Paul Mulagizi ambaye ndugu yake aliuawa.

“Wanatuambua hawajapata idhini ya kuachilia miili. Itatolewa leo, kesho au kesho kutwa?”

Waasi wa kundi la M23 mjini Goma katika mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa Dr Congo, awali Januari. PICHA | REUTERS

Tangu Januari takriban watu 7,000 wameuawa na nusu milioni kuachwa bila makao baada ya kambi 90 za ndani kuharibiwa wakati wa mapigano baina ya M23 na jeshi la DR Congo, kwa mujibu wa serikali.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi jana lilisema kuwa watu 60,000 wametorokea nchi jirani ya Burundi katika wiki mbili zilizopita kukwepa mapigano hayo yanayoshuhudiwa eneo la mashariki lenye utajiri mkubwa wa madini.

Mkutano wa umma Alhamisi ulikuwa wa kwanza wa M23 kuandaa tangu waasi hao wateke mji wa Bukavu majuma machache yaliyopita.

Bukavu ni mji wa pili sasa katika mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa DR Congo kutekwa na M23 baada ya waasi hao kutwaa udhibiti wa mji wa Goma – mkubwa zaidi katika eneo hilo la mashariki.