Kimataifa

Serikali ya Museveni yapitisha kuundwa kwa Baraza Kuu la Kiswahili

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

SERIKALI imeidhinisha hoja ya kutaka kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili litakalotoa mwongozo kuhusu mchakato wa kufanya Kiswahili kuwa lugha rasmi nchini Uganda.

Akihutubia wanahabari kuhusu uamuzi wa Baraza la Mawaziri katika Ikulu ya Rais mjini Entebbe, Msemaji wa Serikali Ofwono Opondo alisema, kubuniwa kwa baraza hilo kunaambatana na matakwa ya katiba.

Alisema baraza hilo litahakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya pili nchini Uganda baada ya Kiingereza.

“Katiba inahitaji kwamba tuwe na lugha mbili za kitaifa; Kiingereza na Kiswahili. Lakini hatujakuwa tukitumia Kiswahili. Baraza hilo litaajiri walimu watakaokuwa wakifundisha Kiswahili shuleni,” akasema.

Alisema baraza hilo pia litasimamia kubuniwa kwa sera, mwongozo na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inafunzwa kwa ubora wa juu.

Bw Opondo alisema baraza hilo pia litahakikisha kuwa Kiswahili kinatumika katika wizara na mashirika yote ya serikali na kutoa vifaa vinavyotakiwa kama vile vitabu na kamusi.

Uganda imekuwa ikitumia Kiingereza kama lugha rasmi tangu nchi hiyo kupata uhuru wake mnamo 1962.

Nchini Uganda, lugha ya Kiswahili ilianza kutumika katika Baraza la Kifalme la Buganda na Bunyoro, hata kabla ya ukoloni (1862). Kiswahili hutumika katika shughuli za biashara, dini na mila.

Nchini Uganda Kiswahili hutumiwa zaidi na Polisi na Wanajeshi.

Katika miaka ya 1980, raia wengi wa Uganda walikiona Kiswahili kama lugha ya wahalifu ikitumiwa na askari kuwadhulumu na kuwanyang’anya mali yao.

Uganda ndiyo nchi ya hivi karibuni kuidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi. Namibia, Rwanda na Afrika Kusini pia zimeidhinisha Kiswahili kufunzwa shuleni.

Baraza la Mawaziri la Namibia liliidhinisha hoja ya kutaka Kiswahili kufunzwa shuleni Julai, mwaka huu.

Serikali ya Namibia ilianza kujadili suala la kufundisha lugha ya Kiswahili baada ya kiongozi wa Tanzania John Magufuli kuzuru nchi hiyo Mei, mwaka huu. Wakati wa ziara yake, Rais Magufuli alitaka Namibia na Tanzania kudumisha ushirikiano ambao umekuwepo tangu 1991 kwa kufundisha Kiswahili.

Magufuli alisisitiza kuwa kulikuwa na haja kwa mataifa hayo mawili kushirikiana katika sekta ya elimu. Kiswahili kitaanza kufunzwa katika shule nchini Afrika Kusini kuanzia mwaka 2020.

Waziri wa elimu msingi, Angie Motshekga mnamo Septemba mwaka jana alisema kuwa, Kiswahili kitafunzwa kama lugha mbadala kwa wanafunzi nchini humo.