Kimataifa

Sudan Kusini yakanusha madai ya Raila

Na JUSTUS OCHIENG April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MZOZO wa kidiplomasia umeibuka kati ya Sudan Kusini na mjumbe maalum wa Kenya, Raila Odinga, baada ya serikali ya Rais Salva Kiir kukataa madai ya waziri mkuu huyo wa zamani kuhusu mgogoro wa kisiasa unaokumba nchi hiyo jirani.

Serikali ya Sudan Kusini ilikanusha madai ya Bw Odinga kwamba Waziri wa Masuala ya Ndani, Angelina Teny, ambaye pia ni mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, alikuwa amezuiliwa nyumbani.

Serikali hiyo pia ilikanusha ripoti kwamba Rais Kiir alimuomba Bw Odinga kuwasiliana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kwa upatanishi.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) aliporejea kutoka safari yake Jumamosi, Bw Odinga alidai kuwa Bw Machar na mke wake, miongoni mwa wengine, walikuwa  wamewekwa katika kifungo cha nyumbani.

“Niliomba kuzungumza na Dkt Machar, lakini hawakuweza kuniruhusu kukutana naye. Badala yake, walinituma nikutane na Rais Museveni, jambo ambalo nilifanya. Kutoka Juba, nilielekea Entebbe,” Bw Odinga alisema.

Lakini katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na katibu wa habari wa Rais Kiir, David Amuor Majur, serikali ya Sudan Kusini ilifafanua kuwa Bw Odinga, kama mjumbe maalum, alipaswa kusafiri kwenda Uganda kumfahamisha rasmi Rais Yoweri Museveni kuhusu matokeo ya mazungumzo yake na Rais Kiir.

“Hata hivyo, Serikali ya Sudan Kusini inahisi kulazimika kufafanua baadhi ya vipengele vya matamshi ya Mheshimiwa Odinga yaliyotolewa baada ya mkutano wake, ambayo hayawakilishi kwa usahihi muktadha au madhumuni ya ziara yake, wala hayazingatii taratibu za kidiplomasia za taifa letu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika maelezo yake, Bw Odinga alisema Bw Machar na mkewe walikuwa katika kifungo cha nyumbani na hakuruhusiwa kuzungumza nao.

Lakini serikali ya Sudan Kusini ilikanusha madai ya Bw Odinga.

“Serikali ya Sudan Kusini inakanusha kwa heshima madai kwamba Mheshimiwa Angelina Teny, Waziri wa Masuala ya Ndani na mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais, yuko katika kifungo cha nyumbani. Madai haya hayana msingi na hayaonyeshi uhalisia wa hali halisi,” serikali ilisema.