Trump akiri Urusi iliingilia uchaguzi wa Amerika 2016
Na AFP
WASHINGTON, AMERIKA
RAIS Donald Trump, alikiri Jumanne kwamba Urusi na ‘nchi nyingine’ ziliingilia uchaguzi wa urais uliofanywa mwaka 2016 ambao alitangazwa mshindi, lakini akaahidi hilo halitawahi kufanyika tena.
Akizungumza kwenye kikao cha wanahabari ambapo aliandamana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, alidai pia kuwa uingiliaji wa Urusi haukuathiri matokeo katika uchaguzi huo.
“Warusi hawakuathiri kura zetu kwa njia yoyote ile lakini kwa hakika, kulikuwa na uingiliaji na pengine pia kutoka kwa nchi nyingine na watu wengine binafsi,” akasema Trump, ambaye amekuwa akipuuzilia mbali ushawishi wa Urusi kwake na amekuwa akipinga vikali madai kwamba wasimamizi wa kampeni zake walishirikiana na Urusi.
Alipoulizwa kama anahofia kitendo hicho kitashuhudiwa tena, rais huyo alisema, “Tutazuia chochote watakachojaribu kufanya kwa kila njia tuwezavyo. Huwezi kukubali mfumo wa uchaguzi kuvurugwa kwa njia yoyote na hatutaruhusu hilo lifanyike.”
Aliongeza: “Hatujasifiwa na mtu yeyote lakini ukweli ni kwamba tunajitahidi sana kuandaa chaguzi zijazo.”
Tisho
Wakati huo huo, rais huyo alikashifu sheria za kibiashara za Muungano wa Ulaya (EU) na kusema muungano huo umefanya iwe vigumu mno kwa kampuni za Amerika kuendeleza biashara zao na akatishia kuongeza ushuru wa bidhaa za mataifa ya EU zinazoingizwa Amerika.
Trump, ambaye ametishia kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa vyuma vinavyoingizwa kutoka nchi za kigeni na asilimia 10 kwa mabati alisema haogopi hata kama kutazuka mgogoro wa kibiashara.
Alionya pia kwamba yuko tayari kuongeza ushuru wa magari ya Ulaya yanayoingizwa Amerika, mengi yakiwa yanatoka nchini Ujerumani.
“Wanafanya iwe vigumu sana kwetu kufanya biashara nao, ilhali wanaleta magari yao na kila kitu kingine Amerika. Wanaweza kufanya chochote kile watakacho lakini wakifanya hivyo, basi tutaweka ushuru mkubwa wa silimia 25 kwa magari yao na mniamini nikisema hawataendelea kwa muda mrefu,” akasema.
Kwa upande wake, Lofven alionya kwamba uhuru na uwazi wa kibiashara ni muhimu sana kwa Sweden na EU.
Aliongeza kuwa ushuru mkubwa utaathiri viwanda vya Ulaya hali wao hutengeneza tu asilimia 10 ya vyuma ulimwenguni huku Uchina ikitengeneza asilimia 50.
“Ninaamini ushuru ukiongezwa tutaumia katika siku zijazo. Hakika, ninaunga mkono juhudi za Uropa kuendeleza biashara chini ya mfumo usiokuwa na vikwazo vingi,” akasema waziri huyo mkuu.