Kimataifa

Uhuru ateuliwa mpatanishi Mashariki mwa DRC

Na JUSTUS OCHIENG’ March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta ataendelea kuwa kati ya viongozi wanaoendeleza juhudi za upatanishi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hii ni baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa yanayopatikana Kusini mwa Afrika (SADC) kuamua aendelee na jukumu hilo.

Bw Kenyatta ataungana na Marais wa zamani Olesegun Obasanjo (Nigeria), Kaglame Motlanthe (Afrika Kusini), Catherine Samba (Jamhuri ya Afrika ya Kati) na Sahle-Work Zewde (Ethiopia).

Kwenye mkutano ulioongozwa na Mwenyekiti wa EAC Rais William Ruto na mwenzake wa SADC Rais Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), SADC, EAC na Umoja wa Afrika (AU), ziliratibisha mkutano na marais hao wa zamani ndani ya siku saba.

Kuafikia kwa orodha ya viongozi hao watano kulizingatia usawa wa kijinsia, kieneo na lugha.

Mkutano ulioandaliwa kupitia teknolojia ya mitandaoni ulihudhuriwa na Rais wa DRC Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame.

Wengine waliohudhuria ni marais Evariste Ndayishimiye (Burundi), Andry Rajoelina (Madagascar), Lazarus Chakwera (Malawi) na Cyril Ramapohosa.

Pia, marais Samia Suluhu (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda) Hakainde Hichilema (Zambia), Waziri Mkuu wa Somalia Hamza Barre, Tete Antonio (Waziri wa Masuala ya Nje wa Angola) na Deng Alor Kuol (Waziri wa Masuala ya Nje wa Sudan Kusini) walihudhuria mkutano huo.

Mawaziri wa EAC- SADC pamoja na makatibu wa SADC na EAC walihudhuria mkutano huo ambao wote walizungumzia hali ya usalama mashariki mwa DRC.

“Mkutano huo uligusia mkutano wa EAC-SADC ulioandaliwa Dar es Salaam Tanzania mnamo Februari 8, 2025 kuhusu hali ilivyo DRC, mapendekezo ya mkutano wa Amani na Usalama wa Baraza la AU mnamo Februari 14, 2025. Pia, mapendekezo ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Kimataifa mnamo Februari 21, 2025 yalijadiliwa,” ikasema taarifa ya EAC-SADC.

Taarifa hiyo ilisema mkutano huo ulisisitiza juhudi za pamoja za kushughulikia usalama unaodorora mashariki mwa DR Congo. Ghasia mashiriki mwa Congo zimekuwa zikitokana na vita kati ya jeshi la nchi hiyo na kundi la M23.

Kundi hilo lilitwaa miji ya Goma, Bukava na Walikate na limeshutumiwa kwa mauaji na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

DRC imedai Rwanda ndiyo imekuwa ikifadhili kundi hilo japo serikali ya Rais Kagame imekanusha madai hayo vikali.