Waandamanaji Sudan wakaidi hali ya hatari
Na MASHIRIKA
WAANDAMANAJI nchini Sudan wamesisitiza kuendelea kukaidi agizo la Rais Omar al-Bashir la kusitisha maandamano dhidi yake baada ya kutangaza hali ya hatari Februari.
Jumatatu, mamia ya waandamanaji walijitokeza kwa wingi katika miji ya Khartoum na Omdurman, huku wakikabiliana vikali na vikosi vya usalama.
Shirika la habari la serikali, SUNA, lilisema watu kadhaa walijeruhiwa, lakini shirika la kutetea haki la Amnesty International lilidai kwamba ghasia zilizuka baada ya vikosi hivyo kuwafyatulia risasi waandamanaji hao.
Rais Bashir alitangaza hali ya hatari iliyotarajiwa kudumu kwa mwaka mmoja mnamo Februari 22, huku akiwapa nguvu maafisa wa usalama kuwakakabili vikali wanaharakati wanaoandaa mikutano yoyote bila kibali kutoka kwa serikali.
Hata hivyo, bunge nchini humo limepitisha hali ya hatari ya muda wa miezi sita tu.
Jumatatu, waandamanaji hao walisisitiza kuendelea na maandamano, wakidai Bashir anatumia agizo hilo la hali ya hatari kama vitisho dhidi yao.
“Bashir hajui kwamba agizo lake limetupa motisha zaidi kuendelea kutetea haki zetu. Utawala wake umegeuka kuwa dhalimu na umesambaratisha msingi wa nchi hii. Hatutatishika hata kidogo,” akasema Ahmed, aliyekuwa miongoni mwa wanaharakati walioshiriki maandamano hayo jijini Khartoum.
Mwandamanaji mwingine alisema kwamba watawashinikiza wenzao kujitokeza kwa wingi zaidi.
“Tulisikia tangazo la Bashir kuhusu agizo mpya ambalo ametoa. Tulingoja kulisikia tukiwa barabarani ili tuweze kumjibu kwa haraka. Hatutatishika hata kidogo,” akasema mwandamanaji mwingine.
Maandamano hayo yamekuwa yakiendelea tangu Desemba 19, 2018.
Inakisiwa kwamba zaidi ya waandamanaji 800 wanazuiliwa na serikali.
Wanaharakati wamekuwa wakimshinikiza kiongozi huyo kung’atuka uongozini kwa madai ya kudorora kwa uchumi.