Wafanyakazi wa serikali wasiofika kazini kukatwa mshahara kila siku wanayosusia
Na VALENTINE OBARA
KAMPALA, UGANDA
SERIKALI itaanza kulipa watumishi wa umma kwa siku ambazo watafanya kazi badala ya kupewa mishahara sawa kila mwezi, afisa mkuu serikalini alisema.
Prof Ezra Suruma ambaye ni mkuu wa Idara ya Utendakazi katika Afisi ya Waziri Mkuu alisema serikali imeanza kuweka mitambo ya kutambua watumishi wa umma kibayometriki hasa katika taasisi za afya na elimu.
Hatua hii imenuiwa kuhakikisha kwamba itajulikana kila wakati mfanyakazi atakapoingia kazini na anapoondoka.
Kulingana na Prof Suruma, mishahara ya watumishi wa umma itakuwa inakatwa kadri na siku ambazo watakosa kwenda kazini.
“Wiki iliyopita tulikuwa Jinja kwa mkutano wa serikali za mitaa na wilaya tukaambiwa kuna wilaya ambazo huwa hazilipi watumishi wa umma wanaokosa kwenda kazini. Tunataka wilaya zingine zifuate mkondo huu,” akasema.
Wilaya za Kaliro, Kayunga, Buvuma, Bulambuli, Bugiri na Bududa zilizo mashariki mwa Uganda tayari zinatekeleza mfumo huu.
Prof Suruma alisema raia ambao hawaridhishwi na huduma za serikali wameanza kuwasilisha malalamishi yao na kuripoti wafanyakazi wa umma wasiopatikana afisini kupitia kwa mitandao ya kijamii hasa WhatsApp.