Kimataifa

Waliofariki katika ajali ni watu 46 wala si 63, maafisa wa Uganda wasema

Na WINNIE ONYANDO na MASHIRIKA October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAMLAKA ya Uganda imesema kuwa idadi ya waliofariki katika ajali iliyotokea kwenye Barabara Kuu ya Kampala–Gulu ni 46 na si 63 kama ilivyoripotiwa na polisi hapo awali.

Hapo awali, maafisa waliripoti kuwa watu 63 waliangamia kwenye ajali hiyo na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Maafisa wanasema baadhi ya waathiriwa waliodhaniwa kuwa wamekufa hapo awali walipatikana wakiwa wamezira na sasa wanatibiwa katika vituo mbalimbali vya afya.

“Tunathibitisha kuwa idadi ya walioangamia katika ajali hiyo iliyohusisha basi, lori na gari dogo aina ya Toyota Land Cruiser iliyotokea katika Barabara Kuu ya Kampala–Gulu ni 46. Maafisa walitangaza idadi kuwa 63 hapo awali kwani kuna wengine waliozirai na wakahesabiwa kama waliofariki,”

“Hata hivyo, tunafanya kila tuwezalo ili kutoa idadi kamili ya walioangamia kwenye ajali hiyo,” ripoti iliyotolewa na mamlaka baadaye ilisema.

Maafisa wa kutoa huduma za dharura wanashirikiana na wenzao wa wizara ya afya kuthibitisha idadi hiyo na kutoa taarifa sahihi huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Ajali hiyo iliyotokea Jumatano asubuhi katika kijiji cha Kitaleba, ilihusisha mabasi mawili, lori na gari dogo aina ya Toyota Land Cruiser, kwa mujibu wa ripoti ya awali ya polisi.

Idadi ya vifo inatarajiwa kupanda kwani baadhi ya abiria wamejeruhiwa vibaya mno.

Rais Yoweri Museveni alituma risala za rambirambi kwa waathiriwa wakati akifanya kampeni za uchaguzi mkuu wa Januari 2026 karibu na eneo ambalo ajali hiyo ilitokea.

Miili ya walioaga dunia ilipelekwa katika makafani ya Kiryandongo ikisubiri kufanyiwa upasuaji.

“Uchunguzi bado unaendelea ili kubaini kilichosababisha ajali hiyo,” alisema Julius Hakiza, msemaji wa polisi katika eneo hilo.Kulingana na ripoti ya polisi, idadi ya walioangamia kwenye ajali za barabara katika nchi hiyo mnamo 2024 ni 15,101.

Ajali hizo zinahusishwa na miundombinu mbovu.