Kimataifa

Wanajeshi 53 wauawa katika shambulio la kigaidi Mali

November 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

BAMAKO, MALI

WANAJESHI 53 wa Mali wameuawa baada ya kituo chao kilichoko Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo kushambuliwa na magaidi, serikali imesema.

Raia mmoja pia aliuawa katika shambulio hilo lililotekelezwa Ijumaa jioni katika kituo cha Indelimane katika eneo la Menaka, karibu na mpaka wa Niger, Waziri WA Mawasiliano wa Mali Yaya Sangare alisema kupitia Twitter.

Shambulio hilo limetajwa kuwa baya zaidi kutekelezwa dhidi ya wanajeshi wa Mali katika siku za hivi karibuni ambapo magaidi wamekuwa wakitekeleza mashambulio nchini humo.

Lakini Bw Sangare  amesema Jumamosi hali imedhibitiwa huku shughuli ya kutambua miili ikiendelea.

“Hali ni tulivu sasa. Na idara ya jeshi na asasi husika za serikali zinaendelea kutambua miili ya waliouawa,” alisema.

Manusura watano wa shambulio hilo walipatikana katika kituo hicho ambacho kiliharibiwa vibaya. Hakuna maelezo zaidi yalitolewa kuhusu tukio hilo.

Serikali ya Mali ilisema maafisa zaidi wa usalama wametumwa katika eneo la tukio kuwasaka wavamizi hao, lakini hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo.

Shambulio hilo linajiri muda wa miezi michache baada ya wanajeshi 40 kuuawa katika mashambulio mawili ya kigaidi yaliyotekelezwa karibu na mpaka wa Burkina Faso.

Hata hivyo, duru zinasema huenda idadi ya waliouawa ni ya juu zaidi.

Raia walifanya maandamano nje ya kambi ya kijeshi katika jiji kuu la Bamako siku moja baada ya kutekelezwa kwa shambulio hilo.

Eneo la Kaskazini mwa Mali limekuwa chini ya udhibiti wa kundi la kigaidi lenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda baada ya jeshi la Mali kufeli kuzima maasi katika eneo hilo mnamo 2012.

Majeshi ya Ufaransa yalianza kampeni ya kukabiliana na wafuasi wa kundi hilo la kigaidi na kuwasukuma lakini magaidi hao wakarejea mwaka mmoja baadaye.