Kimataifa

Watu 100,000 wahama moto ukizidi Amerika

Na REUTERS January 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LOS ANGELES, AMERIKA

WATU wasiopungua watano walifariki, huku mamia ya nyumba zikiharibiwa baada ya moto kuteketeza maeneo ya Los Angeles na kuenea hadi Hollywood mnamo Jumatano, Januari 8, 2025 na kukwamisha rasilimali za kuzima moto na usambazaji wa maji.

Meya wa Los Angeles, Karen Bass, alilazimika kukatiza safari rasmi nchini Ghana na kuamrisha watu zaidi ya 100,000 kuhama baada ya upepo mkali na kimbunga, kuzuia juhudi za kuzima, na kusambaza moto huo, ambao umeharibu maelfu ya ekari tangu ulipoanza siku ya Jumanne, Januari 7, 2025.

“Moto huu ni mkubwa sana,” alisema Bass katika mkutano na waandishi wa habari.

Mkuu wa Zimamoto, Kristin Crowley alisema moto mwingine ulizuka katika eneo la Hollywood lenye vilima vilivyokauka Jumatano jioni na kutetekeza ekari 50.

Idara hiyo ilitoa agizo la uhamisho kwa watu katika eneo la Hollywood Boulevard Kusini, Mulholland Drive Kaskazini, Barabara kuu ya 101 Mshariki, na Laurel Canyon Boulevard Magharibi, maeneo maarufu kwa sekta ya burudani.

Crowley aliongeza idadi ya mioto inayowaka katika Kaunti ya Los Angeles ilifikia sita.

Maafisa wa serikali walisema nne kati ya mioto sita iliyotokea, haikudhibitiwa, ikiwemo mikasa miwili mikubwa kwenye pande za Mashariki na Magharibi mwa jiji ambayo iliendelea kuongezeka usiku wa Jumatano.

Hali hiyo, ilisababisha watu watatu kukamatwa kwa tuhuma za uporaji.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Dharura wa Los Angeles Kevin McGowan, alisema kampuni binafsi ya utabiri wa hali ya hewa ya AccuWeather ilikadiria hasara ya zaidi ya Sh6 trilioni.

“Tunashuhudia janga la asili la kihistoria. Nadhani hili haliwezi kusemwa kwa nguvu zaidi,” alisema McGowan.

Ingawa, watabiri walisema upepo ungetulia kidogo usiku wa Jumatano, maeneo yanayojulikana kuwa hatari yalitazamiwa kuendelea hadi Ijumaa.

Mkurugenzi wa Ubunifu kutoka Topanga, Jaye Riedinger, 37 alisema kuwa farasi na wanyama wengine waliokuwa wakipata hifadhi katika kituo cha farasi cha chuo walipelekwa sehemu salama.

Taarifa kutoka kwa PowerOutage.us, ilisema kuwa nyumba na biashara 300,000 zilipoteza umeme katika Kaunti ya Los Angeles, idadi hiyo ikishuka kutoka milioni moja kama ilivyokuwa imetangazwa awali.

Moto huo uliathiri watu mashuhuri ambao walipoteza nyumba zao.

Zaidi ya majengo 1,000 yaliharibiwa, yakiwemo majumba ya wasanii wa filamu za Amerika almaarufu Hollywood.