Kwa kila bao atakalofunga Salah, tutawapa wateja wetu dakika 11 za maongezi bila malipo, yasema Vodafone Misri
Na GEOFFREY ANENE
WATEJA wa kampuni ya mawasiliano ya Vodafone nchini Misri wamo mbioni kupata dakika 11 za bure za mjazo wa simu.
Kwa mujibu wa tovuti ya 101 Great Goals, zawadi hii itategemea makali ya Mohamed Salah mbele ya goli kwa sababu ofa yenyewe itakuwa hai tu ikiwa mvamizi huyu matata ataendelea kuchana nyavu katika mechi zilizosalia msimu 2017-2018.
Kampuni hiyo iliteua dakika 11 kutokana na nambari ya jezi ya Mohamed Salah mgongoni.
Vodafone, ambayo mwaka 2017 iliripotiwa kuwa na wateja 43 milioni nchini Misri, ilitangaza Machi 20, 2018 kwamba kila wakati Salah atafunga bao, wateja wake watapokea mjazo wa simu wa dakika 11 za bwerere.
Mwanasoka huyu bora wa Afrika mwaka 2017 amekuwa akitesa wapinzani vilivyo msimu huu kwa kutikisa nyavu na pia kumega pasi za uhakika zilizozalisha mabao.
Salah, 25, amefungia Liverpool mabao 28 katika mechi 31 imecheza kwenye Ligi Kuu msimu huu. Pia amemegea wachezaji wenzake pasi 10 ambazo zimezalisha mabao.
Vilevile, Salah amesaidia Liverpool kuingia robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kutikisa nyavu mara sita na kumega pasi mbili zilizojazwa kimiani.
Katika mechi iliyopita, Salah alipachika mabao manne Liverpool ilipozamisha Watford 5-0 Machi 17 uwanjani Anfield.
Kwenye Ligi Kuu, Salah anahitaji mabao mawili pekee kufuta rekodi ya mfungaji wa mabao mengi katika msimu mmoja kutoka Bara Afrika. Raia wa Ivory Coast, Didier Drogba anashikilia rekodi hiyo ya mabao 29 aliyofungia klabu ya Chelsea msimu 2006-2007.
Salah pia anakaribia kufuta rekodi za mabao 34 katika msimu mmoja zilizowekwa na Andy Cole (Manchester United, 1993-1994) na Alan Shearer (Blackburn Rovers, 1994-1995) wakati ligi ilikuwa na klabu 22. Wakati huu, ligi inajumuisha timu 20.
Ratiba ya mechi za Liverpool zilizosalia msimu 2017-2018:
Machi 31 – Crystal Palace vs. Liverpool (Ligi Kuu)
Aprili 4 – Liverpool vs. Manchester City (Robo-Fainali ya Klabu Bingwa mkondo wa kwanza)
Aprili 7 – Everton vs. Liverpool (Ligi Kuu)
Aprili 10 – Manchester City vs. Liverpool (Robo-Fainali ya Klabu Bingwa mkondo wa pili)
Aprili 14 – Liverpool vs. Bournemouth (Ligi Kuu)
Aprili 22 – West Brom vs. Liverpool (Ligi Kuu)
Aprili 28 – Liverpool vs. Stoke (Ligi Kuu)
Mei 5 – Chelsea vs. Liverpool (Ligi Kuu)
Mei 13 – Liverpool vs. Brighton (Ligi Kuu)