MADENI: Kenya hatarini kupigwa mnada na Uchina
PATRICK ALUSHULA Na VALENTINE OBARA
Kwa muhtasari:
- Huenda Uchina ikatwaa Bandari ya Mombasa, JKIA, Reli ya SGR na ardhi Kenya ikilemewa kulipa madeni
- Uchina imewahi kuchukua hatua kama hii wakati serikali ya Tajikistan ilipoikabidhi ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 286,000 iliposhindwa kulipa madeni yake kwa wakati ufaao
- Hatari iliyopo inatokana sana na makubaliano kati ya Kenya na Uchina kukosa uwazi kuhusu jinsi madeni yatakavyolipwa
KENYA imo kwenye hatari ya kupokonywa rasilimali zake muhimu na Uchina kutokana na madeni yake mengi kwa nchi hiyo, shirika la uchanganuzi wa masuala ya kifedha kimataifa limeonya.
Takwimu za Wizara ya Fedha zinaonyesha kuwa kufikia Septemba, madeni ya Kenya kwa Uchina yalifika Sh554.88 bilioni, na ikikosa kulipa kwa wakati huenda Uchina ikatwaa usimamizi wa Bandari ya Mombasa, viwanja vya ndege kama vile JKIA ama Moi mjini Mombasa, Reli ya SGR, ardhi ama raslimali zingine.
Kutokana na deni kubwa ambalo Uchina inadai Kenya, shirika la kuchanganua masuala ya kifedha kimataifa la Moody’s Investor Service limeorodhesha Kenya miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo zimo katika hatari ya kupoteza rasilimali kama zitashindwa kulipa madeni hayo kwa wakati ufaao.
“Mataifa yaliyo na utajiri wa mali asili kama vile Angola, Zambia na Jamhuri ya Congo, au yaliyo na rasilimali muhimu kama vile bandari na reli kwa mfano ilivyo Kenya, yako katika hatari kubwa zaidi ya kupokonywa udhibiti wa mali hizo,” ripoti ya Moody’s imeonya.
Uchina imewahi kuchukua hatua kama hii wakati serikali ya Tajikistan ilipoikabidhi ardhi yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 286,000 iliposhindwa kulipa madeni yake kwa wakati ufaao.
Hatua sawa na hii ilichukuliwa nchini Sri Lanka ambapo Uchina ilitwaa usimamizi wa Bandari ya Hambantota.
Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitetea madeni yanayochukuliwa na serikali yake akisema Kenya inahitaji fedha hizo kuimarisha miundomsingi yake kwa minajili ya kustawisha maendeleo yatakayoboresha maisha ya wananchi.
Mbali na Moody’s, mashirika mengine tajika ya kifedha na vilevile wataalamu binafsi wa masuala ya kiuchumiwamekuwa wakionya serikali dhidi ya kuchukua mikopo mingi ambayo inaweza kushinda wananchi kulipia.
Kulingana na ripoti ya Moody’s, hatari iliyopo inatokana sana na makubaliano kati ya Kenya na Uchina kukosa uwazi kuhusu jinsi madeni yatakavyolipwa.
Mataifa kama vile Kenya na Uganda, ambayo hayana bidhaa nyingi za kuletea nchi mapato ya kigeni, yanaweza kulemewa na madeni hayo.
Zaidi ya hayo, ilisema madeni ya Uchina hupeanwa kwa mataifa bila kuzingatia uadilifu wa matumizi ya fedha hizo na hivyo basi malengo ya maendeleo yanaweza kukosa kuafikiwa na hii itaathiri vibaya uchumi wa nchi ambayo bado itahitajika kulipa madeni yake.
Hali hii ni tofauti na mikopo inayochukuliwa kutoka kwa Benki ya Ulimwengu na Muungano wa Ulaya, ambazo huhitaji thibitisho la serikali kwamba sera za uongozi bora, maendeleo ya kijamii na demokrasia zitafuatwa kikamilifu.