Mbadi, Duale na Migos kukutana na wabunge wakipanga ajenda ya 2026
MAANDALIZI ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 pamoja na changamoto zinazokumba utekelezaji wa mfumo wa Elimu ya Umilisi (CBE), ni kati ya ajenda kuu zitakazojadiliwa na wabunge mjini Naivasha kuanzia Jumatatu.
Wawakilishi wote wa Bunge la Kitaifa watakutana Naivasha kwa mkutano wao wa kila mwaka, ambao pia utajadili mustakabali wa Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF), wiki moja kabla Bunge kufunguliwa tena Februari 10
.
Mbali na masuala ya uchaguzi na mpito wa wanafunzi kujiunga na sekondari pevu katika Gredi 10 – ya kwanza chini ya CBE wabunge pia watakutana na Waziri wa Fedha John Mbadi na mwenzake wa Afya Aden Duale kujadili hali ya uchumi na utoaji wa huduma za afya nchini.
“Taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao, mfumo wa kisheria na kifedha unaosimamia vyama vya kisiasa unahitaji kupigwa darubini upya na Bunge ili kulinda uaminifu wa uchaguzi, haki na uthabiti wa kisiasa,” waraka wa Bunge kuhusu mkutano unasema.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon anatarajiwa kufika Naivasha Jumanne ili kuwapa tathmini ya maandalizi ya tume kuendesha uchaguzi wa kuaminika mwaka 2027.
“Mkutano huu utawapa wabunge fursa ya kuhoji IEBC na taasisi nyingine husika, kwa kuzingatia hali ya mipaka ya kiuchaguzi, usajili na elimu ya wapigakura, teknolojia ya uchaguzi, na mifumo ya kisheria na sera,” Bunge limesema.
Kuhusu utekelezaji wa CBE, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba atafika mkutanoni Jumatano kupambanua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wadau wa elimu hususan kuhusu miundombinu ya shule, maandalizi ya walimu, ufadhili na mgawo wa walimu kwa wanafunzi kadri wanavyopanda madarasa.
Bw Ogamba atazungumzia mada ya ‘Mpito kutoka Sekondari Msingi hadi Sekondari Pevu, Ufadhili, Ujenzi wa Miundombinu ya Shule na Maandalizi ya Walimu’.
Waraka wa Bunge waeleza: “Kikao hiki kitawapa wabunge fursa ya kutathmini hali ya sasa ya utekelezaji wa CBE na utayari wa taasisi za serikali kushughulikia changamoto ibuka, kwa lengo la kubaini sera na kisheria zinazohitajika ili kuimarisha utekelezaji endelevu wa mtaala,” Bunge limesema.
Kuhusu hali ya uchumi, Bw Mbadi atafahamisha wabunge kuhusu mazingira ya sasa ya kiuchumi huku kukiwa na shinikizo kwa bajeti na ongezeko la mahitaji ya huduma za umma.
Kuhusu Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Bw Duale atakabiliwa na maswali kuhusu hali ya sekta ya afya hasa utoaji wa huduma chini ya SHA katika usimamizi wa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).
Majadiliano hayo yatakayofanyika katika wakati muhimu wa Bunge la sasa pia yatatoa fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa hadi sasa na kuzingatia hatua za sera au sheria zinazohitajika kuunga mkono Hazina ya Kitaifa.