Mikono fiche iliyomnusuru Nyaribo
GAVANA wa Nyamira Amos Nyaribo amewaambia wakosoaji wake waache masengenyo na wamakinike maendeleo kwa umma baada ya kunusurika jaribio la tatu la kuondolewa mamlakani.
Bw Nyaribo alinusurika Jumatano usiku baada ya maseneta kupiga kura ya kutupilia mbali hoja iliyolenga kumng’atua madarakani.
“Nawaomba viongozi wenzangu tutatue masuala yetu nyumbani badala ya kuyaleta hapa kwenye Seneti,” akasema Bw Nyaribo baada ya kuokolewa na Seneti.
Kuna madai kwamba Bw Nyaribo aliokolewa na Ikulu pamoja na wanasiasa wa Gusii ambao wanaegemea mrengo wa serikali.
Hata hivyo, amekanusha kuwa Ikulu ilikuwa na mkono katika kuponyoka kwake.
Kinaya ni kwamba baadhi ya wanaodai walimnusuru Bw Nyaribo ndio wale walishirikiana na madiwani ili aondolewe madarakani.
Walinakiliwa wakiwaambia madiwani wamtimue gavana huyo.Mkesha wa uamuzi dhidi yake, baadhi ya wanasiasa wa UDA akiwemo Dennis Itumbi, walikuwa wamesema kuwa Bw Nyaribo alikuwa amekubali kushirikiana na Serikali Jumuishi kwa hivyo hangeondolewa na Seneti.
“Nitaendelea kupigania umoja wa jamii ya Abagusii. Maseneta kutoka mirengo yote ya kisiasa walikubali kuwa niling’atuliwa kinyume cha sheria na wanne pekee ndio walipinga,” akasema Bw Nyaribo huku akikanusha kuwa alikuwa amejiunga na Serikali Jumuishi.
Baadhi ya wandani wa gavana huyo wanasema nia ya kung’atuliwa kwake ilikuwa kumtishia tu aunge mkono Serikali Jumuishi wala si kufurushwa kabisa madarakani.
“Ilikuwa njama ya kumshinikiza aunge Serikali Jumuishi. Yeye ni kati ya viongozi wakuu wanaomuunga mkono Dkt Fred Matiang’i na hilo limewakasirisha baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi,” akasema mmoja wa wanasiasa ambao wanafahamu kwa kina kinachoendelea kwenye siasa za Kaunti ya Nyamira.
Kabla ya kuanza kwa vikao vya kusikizwa kwa hoja dhidi ya Bw Nyaribo kwenye seneti, gavana huyo alionekana kwenye picha akiwa na Gavana Simba Arati nyumbani kwake Mtaa wa Lavington, Nairobi.
Kwenye picha hiyo pia alikwepo Mbunge wa Mugirango Kusini na Kiranja wa Wengi Silvanus Osoro na Mwekahazina wa UDA Japheth Nyakundi.
Picha hizo ziliibua madai kuwa Bw Nyaribo amekubali kuinga Serikali Jumuishi.
Wengine walidai Bw Arati alikuwa akitumia masaibu ya kisiasa ya Bw Nyaribo kujiinua kisiasa.
Nao wandani wa Bw Nyaribo walimshukuru Bw Arati kwa kusimama na nduguye lakini hawakufafanua matamshi hayo.
Duru hata hivyo zinaarifu kuwa gavana huyo wa Kisii aliwashawishi maseneta wa ODM wapige kura ya kumwokoa Bw Nyaribo.
“Siku hizi kuondolewa kwa gavana mamlakani ni suala la kisiasa kuliko sheria. Kwa hivyo, lazima uwashawishi wanasiasa na sheria ifuatwe ili usiadhibiwe,” akasema mmoja wa wandani wa Bw Nyaribo.
Sasa swali kuu ni iwapo gavana huyu wa Nyamira atasalia kwenye kambi ya Dkt Matiang’i au mwishowe ataungana na kambi ya Serikali Jumuishi.