Mishahara ya maafisa wa polisi haifai kupunguzwa – KNCHR
Na CECIL ODONGO
TUME ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, (KNCHR) Jumatatu imekejeli vikali ripoti kwamba mshahara wa maafisa wa polisi umepunguzwa na kuitaja kama hatua isiyofaa.
Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Kagwira Mbogori amesema idara ya polisi imekuwa ikitekeleza majukumu muhimu ya kudumisha amani na hatua hiyo itaathiri mno mageuzi ambayo yamekuwa yakiendelezwa na tume ya huduma kwa polisi.
Maafisa wa polisi ambao tayari washapokea mishahara yao ya mwezi Machi waliambia Taifa Leo kuwa akaunti zao zilionyesha mishahara iliyopunguzwa kwa hadi Sh26,000.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume ya Huduma kwa polisi Bw Johnstone Kavuludi amekanusha ripoti hiyo na kusema kwamba hakuna afisa aliyekatwa wala kupunguziwa mshahara.
Akiongea mjini Kitale, Bw Kavuludi alisema kile walikuwa wakifanya ni ukaguzi na utambuzi ili kila afisa awe akipokea mshahara anaostahili.
“Kuna maafisa ambao hawajawasilisha vyeti vya kuhitimu stashahada na shahada lakini wanapokea mshahara wa afisa wa cheo cha konstebo, hao ndio tunapambana nao,” akasema.
Kwa upande wake Bi Mbogori alitetetea tume yake kuhusu dhana machoni pa umma kwamba wao hupigania tu maslahi ya raia wanaodhulimiwa na polisi na kukosa kuwajibika haki za polisi wenyewe.
“Sisi tunaangazia haki za maafisa hao jinsi tunavyoshughulikia raia wanaodhulumiwa. Kwa sasa tuna kesi kadhaa ambazo tunafuatilia kuhusu raia waliowavamia polisi kipindi cha kabla na baada ya uchaguzi,” akasema.
Aidha alidai kwamba baadhi ya changamoto zinazokabili polisi ni kukosa kulipwa marupurupu yao, ukosefu wa bima ya afya inayoeleweka na muda mrefu wa kutolewa kwa pesa za maafisa wanaofariki wakiwa kazini.
Aliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Nasa Raila Odinga kwa kuamua kushirikiana kisha akawataka kuipa kipaumbele swala la fidia kwa jamaa ya waliofariki na waliojeruhiwa wakati misururu ya maandamano baada na kabla ya uchaguzi wa marudio Oktoba 26.
“Wakati wa kurejea kwa Raila tuliona ukatili mkubwa wa maafisa wa polisi. Walitekeleza mauji na kutumia nguvu kupita kiasi,” akaongeza.
Bi Mbogori alikuwa akizungumza katika makao makuu ya tume hiyo iliyoko barabara ya Lenana wakati wa kutoa ripoti ya kila mwaka kuhusu hali halisi ya nchi uhuru na haki za raia zikiangaziwa.
Maswala mengine yanayoathiri nchi aliyoyagusia ni utekelezaji kikamilifu wa ripoti ya Tume ya Haki Ukweli na Maaridhiano, utunzaji wa mazingira, uhuru wa vyombo vya habari, ufisadi katika serikali za kaunti na kulemazwa kwa masomo katika kaunti ya Wajir kutokana na hali mbovu ya usalama.