Msamaha wa Atwoli wakosa kutuliza joto
Na BENSON AMADALA na DERICK LUVEGA
MSAMAHA wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, kwa kinara mwenza wa NASA, Bw Musalia Mudavadi, umeonekana kukosa kutuliza hasira ya wabunge waliokasirishwa na hatua ya kiongozi huyo kukosa kuhudhuria hafla ya kiapo cha Raila Odinga.
Bw Atwoli na Bw Mudavadi walitangaza Jumapili kwamba wameamua kushirikiana baada ya kufanya mkutano faraghani na wazee wa jamii ya Waluhya katika eneobunge la Khwisero.
Hapo Jumatatu, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, na Mbunge Maalumu Godfrey Otsosi walisisitiza kuwa maelewano ya wawili hao ni “kiraka” tu kwenye tatizo kubwa la kisiasa ambalo limesababisha mgawanyiko katika Chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Mudavadi.
Mbali na wawili hao, Mbunge wa Vihiga, Bw George Khaniri, pia amekuwa akimkashifu Bw Mudavadi hadharani kwa kukosa kuhudhuria hafla hiyo iliyofanyika Januari 30, katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.
Bw Malala alisema Bw Mudavadi anafaa kujitafutia umaarufu kitaifa badala ya kutegemea wazee wa jamii ya Waluhya kama kweli anataka kuwania urais mwaka wa 2022.
Aliwalaumu baadhi ya wandani wa Bw Mudavadi akidai wanampotosha kuhusu masuala muhimu yanayoathiri ANC na muungano wa NASA kwa jumla.
“Ingawa hatua hiyo ya wazee inaridhisha, inaonekana kama mbinu iliyonuiwa kupuuzilia mbali suala muhimu kuhusu kwa nini Bw Mudavadi hakuonekana wakati wa kuapishwa kwa Bw Odinga,” akasema Bw Malala.
Kutumiwa na Jubilee
Wanasiasa hao watatu walikashifiwa vikali na wenzao wanaounga mkono hatua za Bw Mudavadi, ambao walidai wanatumiwa na chama tawala cha Jubilee kuvuruga upinzani.
Hata hivyo, Bw Otsosi alisema wale wanaowashutumu kwamba wanatumiwa na Jubilee si waaminifu.
“Hatutaomba msamaha wowote kwa kuuliza kwa nini Bw Mudavadi na wabunge hao hawakuwepo Uhuru Park kushuhudia Bw Odinga akiapishwa kuwa “rais wa wananchi,” akasema Bw Otsosi.
Wachanganuzi wa kisiasa katika eneo la magharibi walionekana kukubali kwamba upatanisho wa Bw Atwoli na Bw Mudavadi hautaleta mabadiliko makubwa kama bado kuna matatizo chamani.
Bw Martin Andati, mchanganuzi wa kisiasa, alisema Bw Mudavadi alifanya kosa kisiasa kwa kutohudhuria hafla ya kiapo.
Yachekesha
“Inachekesha kwa sababu Bw Atwoli alikuwa amesema Bw Mudavadi ni mwoga na akaapa kutomuunga mkono tena kisha sasa anasema hayo yote yamepita?” akauliza.
Kwa upande wake, mchanganuzi mwingine, Bw Joseph Simekha, alisema Bw Mudavadi yuko hatarini kutotazamwa kama kiongozi wa kitaifa kama atazidi kutangazwa kama kinara wa Waluhya.
“Bw Mudavadi anafaa awe na wasiwasi kuhusu wafuasi wake na wala si kuhusu msimamo wa Bw Atwoli. Wafuasi wake walihisi kuchezewa shere,” akasema.