Habari

Mtoto alivyoibwa baada ya kuzaliwa, hospitali lawamani

January 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

WINNIE ATIENO, MOMBASA

Bi Victoria Zubeida (pichani) alitembea katika Kituo cha Matibabu cha Mikindani huko Jomvu, Kaunti ya Mombasa Jumapili jioni baada ya kupata maumivu makali ya kujifungua.

Saa tano za usiku, alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume. Walakini, madaktari walimlaza mtoto, wakisema alikuwa na kasoro.

DAWA ZA MTOTO

Siku ya Jumanne, karibu saa kumi jioni, Bi Zubeida, 25, alikutana na mwanamke mwingine mjamzito.

“Aliniuliza kuhusu huduma hospitalini na tuliongea kwa muda mrefu. Mume wangu alifika na kuwasihi madaktari kuturuhusu kwenda nyumbani baada ya afya ya mtoto wetu kuimarika, lakini walisema hali yake bado haijabadilika,” alisema.

Lakini saa moja jioni, Bi Zubeida anasema aliruhusiwa kutoka hospitalini.

“Niliondoka bila kusaini chochote, na yule mama akajitolea kunisaidia. Muuguzi aliniambia atanipa dawa za mtoto, lakini niliondoka haraka. Alipofika kituoni cha basi, mwanamke huyo alinikumbusha juu ya dawa hizo kwa haraka nikarudi, nikamwacha na mtoto wangu,” alisimulia.

Hakujua kilichokuwa mbele, alikimbilia hospitalini na akakusanya dawa kutoka kwa muuguzi lakini, aliporudi kwenye kituo cha basi, hakuweza kumpata yule mwanamke na mtoto. Alianguka na kulia. 

Baada ya dakika chache, msamaria mwema alimpeleka hospitalini ili kuuliza ni nini kilichotokea.

Lakini hospitali ilikataa kumsikiza nje, kulingana na wakazi wa Mikindani wakiongozwa na Bi Joyce Adhiambo na Bw Wafula Wamangey. Walisema walimsihi mlinzi wa hospitali hiyo amruhusu mwanamke huyo mwenye shida apumzike katika kituo hicho baada ya kulia sana.

“Lakini walikataa. Mumewe alifika karibu saa mbili za usiku. Alikasirika sana na alitaka kumpiga, akidai mtoto alikuwa ameuzwa. Ilibidi tuingilie kati na kumtuliza, “akasema Bw Wamangey. Alishuku kuchezewa karata na hospitali inapaswa kushtakiwa, alisema.

KUFUNGIWA NJE

“Je! mgeni huyo aliwezaje kuingia wadi ya akina mama? Tunayo maswali ambayo usimamizi wa hospitali lazima ujibu. Wangewezaje kumfungia mgonjwa wao akilia nje ya hospitali usiku wa manane? ” aliuliza.

“Walimwacha mama huyu nje ya kituo akilia. Wasimamizi walikuja na hawakusema neno. Tuliwasihi wamruhusu alale katika nyumba, lakini walikataa, ” akaongeza.

Mume wa Zubeida, Bw David Muya, alishindwa kuongea.

”Jumatatu asubuhi, nilikuja kuwaona mtoto wangu na mke wangu na tuliambiwa bado alikuwa mgonjwa. Siku ya Jumanne karibu saa sita mchana, nilipeleka majirani zangu kumsaidia mke wangu ili akiruhusiwa kwenda nyumbani waje naye lakini madaktari walisisitiza mtoto bado alikuwa mzuri. ”

Bw Muya alikwenda hospitalini na kupata mkewe analia nje ya kituo usiku.

PICHA ZA CAMERA YA CCTV

“Niliwaambia madaktari wasimruhusu kwenda nyumbani mke wangu wakati yuko peke yangu; anapaswa kuambata nami au majirani zangu. Kwa nini walimtupa usiku? Ni nani aliye saini fomu za kuondoka hospitalini? Je! Kwa nini walibadilisha tarehe ya kuzaliwa ya mtoto wangu kutoka Jumapili hadi Jumanne” aliuliza huku machozi yakimtiririka.

Bw Muya alisema mkewe aliulizwa abadilishe tarehe za kuzaliwa za mtoto wake kwa sababu maelezo muhimu hayakuwa yamesajiliwa katika Kadi ya Bima ya Taifa (NHIF).

“Waliniambia ikiwa nataka NHIF isimamie matibabu yangu, lazima nibadilishe tarehe. Hizi zote ni ishara. Wameiba mtoto wangu, ilikuwa tu ujanja, ” alisema Bi Zubeida, ambaye aliripoti jambo hilo katika kituo cha polisi cha Mikindani.

“Niliwasihi madaktari watupatie nakala ya CCTV ya kumtafuta mwanamke aliyekimbia na mtoto wangu, lakini hospitali imebaki kimya,” alisema.

Wakazi sasa wanataka serikali ya kaunti ichunguze hospitali. Jaribio letu la kutafuta majibu kutoka kwa hospitali lilizuiliwa na maafisa wa usalama, ambao walitufungia nje ya kituo hicho.

Lakini kamanda wa kaunti ndogo ya Jomvu, Bw Jashon Polloh alisema uchunguzi kuhusu kisa hicho umeanzishwa.

Imetafsiriwa na Sammy Kimatu