Habari

Mvua yavuruga shughuli Kitengela na kuanika muundomsingi mbovu

Na  STANLEY NGOTHO January 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MVUA kubwa ambayo imenyesha siku mbili katika Kaunti ya Kajiado ilisambaratisha shughuli za uchukuzi na biashara kwenye mji wenye shughuli nyingi wa Kitengela.

Sehemu ya barabara inayotoka mzunguko wa benki ya KCB na kichinjio kikubwa mjini humo ilijaa maji na kuzima shughuli za uchukuzi.

Jumatatu asubuhi kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara hiyo.

Magari yakipambana na barabara mbovu mjini Kitengela kufuatia mvua kubwa Jumatatu, Januari 27, 2025. Picha|Stanley Ngotho

Kutokana na kuwa na mabomba mabovu ya majitaka, takataka zilitapakaa kote majini. Wakazi walilalamika kuwa kila mara mvua inaponyesha mjini humo, huwa kuna mafuriko makubwa na barabara huwa hazipitiki.

Gari laingia kwenye kidimbwi cha maji ya mvua Kitengela Jumatatu, Januari 27, 2025. Picha|Stanley Ngotho

Baadhi ya bidhaa ambazo zilikuwa kwenye maeneo ya kibiashara nazo zilisombwa, wafanyabiashara wakipata hasara tele.

“Serikali ya Kaunti ya Kajiado imelala kazini. Sisi ni walipa ushuru lakini hatupati thamani na huduma za pesa zetu,” akalalamika George Onyango.