Habari

Nakuru: Mji usiotambua Leba Dei, hapa kazi tu!

May 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA PETER MBURU

HUKU wafanyakazi kote nchini wakipumzika kuadhimisha siku ya Leba Dei Jumanne, Wakenya wengi wanaofanya kazi za juakali na wafanyabiashara ndogondogo wako kazini mjini Nakuru.

Hii, kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo, ni kutokana na hali ngumu ya maisha na kuadimika kwa pesa, ambako kumewasukumia wakenya kukumbana na maisha magumu na kuwalazimu kuwa kazini hata siku ambazo kwa kawaida huwa za likizo.

Wakenya wanaofanya kazi za bodaboda, wauzaji wa nguo, wauzaji wa vyakula, wachuuzi mbalimbali na hata wamiliki wa maduka walikuwa kazini, huku wakijikaza kutafuta pesa za kukimu maisha yao.

Kwa wakazi hawa wa mji wa Nakuru, kuhudhuria sherehe za Leba Dei kisha kurudi nyumbani bila hela ni jambo lisilowaingia akilini hata kidogo. Picha/ Peter Mburu

Mjini Nakuru, takriban asilimia 95 ya biashara zisizo za ofisi zimefunguliwa, huku waliohojiwa na Taifa Leo wakieleza kuwa hawana mengi ya kusherehekea kiasi cha kuwacha kazi zao waende wakaadhimishe sikukuu hii.

“Kwa kweli ningependa kupumzika kama watu wengine ili pia name nisherehekee sikukuu lakini namna hali ya maisha imekuwa ngumu na pesa kukosa nimelazimika kuwa kazini,” akasema Bi Margaret Wanjiru, muuzaji wa vyakula sokoni mjini Nakuru.

Bw Jackson Mwangi ambaye ni mhudumu wa Bodaboda mjini humo alisema kuwa hangeweza kupumzika kazini kusherehekea sikukuu, hasa akikumbuka mwezi ulipo na kuwa anahitajika kulipa kodi ya nyumba.

Wanabodaboda walikuwa kazini angalau kusaka hela za kujikimu maisha Mei 1, 2018. Picha/ Peter Mburu

Bw Mwangi hakuwa peke yake kwani wahudumu hao walifurika mjini, wakitoa ishara kuwa sekta hiyo japo imechangia kukua kwa uchumi vikubwa nchini, wafanyabiashara wake bado wanapigana na ugumu wa maisha.

“Ni vigumu kupumzika wakati huu kwanza kwa kuwa shule zinafunguliwa na kama wazazi tunahitajika pesa ili watoto warejee shuleni. Wakati huu tunapambana kupata pesa kwani kwa muda mrefu maisha yamekuwa magumu,” akasema Bw Charles Ndirangu, muuzaji wa nguo.

Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa wakazi wengi wa Nakuru walikosa kuhudhuria sherehe za Leba Dei Nakuru katika uwanja wa Afraha, wa juakali wakisalia kazini na wale wa maofisini wakisalia manyumbani.