HabariSiasa

Ndoa ya NASA yaingia doa: ODM yampiga Wetang'ula mjeledi

March 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na LUCY KILALO na IBRAHIM ORUKO

CHAMA cha ODM kimemuondoa Seneta wa Moses Wetangula kama kiongozi wa Wachache katika Seneti, hatua ambayo huenda ikaashiria kuwa ndoa ya muungano wa NASA imesambaratika kabisa.

Chama hicho kilimwandikia barua Spika wa Seneti, Kenneth Lusaka kikieleza kuwa nafasi hiyo sasa itashikiliwa na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo.

Spika baadaye alikubali ombi hilo na kusema lilifuata kanuni zote. Uamuzi huo ni kinyume na awali ambapo alikuwa ametoa pingamizi.

Hata hivyo, Seneta Wetang’ula ambaye ni kinara mwenza katika muungano huo na kiongozi wa chama cha Ford Kenya, aliapakutobanduka huku akionya ODM kuwa ndoa hiyo “itavunjika kwa fujo”.

“Ikiwa mnataka talaka, basi lazima muwe tayari kwa sababu itakuwa na vurumai na haitakuwa rahisi,” alisema.

Seneta huyo wa Bungoma alimshtumu mwenzake Bw Orengo kwa kupanga njama hiyo ya kumuondoa.

Kiranja wa Wachache, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, aliwasilisha barua hiyo kwa spika, ambapo alielezea kupokea kumbukumbu za mkutano wa chama cha ODM wa Machi 14, ambapo maseneta 16 waliidhinisha uamuzi huo.

Spika Lusaka alifafanua jana kwamba utaratibu kulingana na kanuni ambayo imeonyesha mkutano ulifanywa, kuna kumbukumbu na kuna maseneta waliotia saini, Seneta Wetangula ameondolewa kihalali kutoka kwa afisi hiyo.

Hata hivyo, alieleza kuwa Seneti inatambua muungano wa NASA na si chama cha ODM, kwa kuwa awali ilijitambulisha hivyo, matakwa ya kanuni ya bunge hayajatimizwa, na hatua hiyo itasimamishwa hadi “seneta aliyechaguliwa na Muungano wa NASA kwa njia ambayo imeelezwa na Kanuni 20(1) ya Bunge na mawasiliano kuhusiana nao, pamoja na kumbukumbu kuonyesha ushahidi kwamba uamuzi umefanywa kwa kuandika barua kwa afisi yangu na Kiranja wa Wachache wa Seneti.”

Uhusiano baina ya ODM na vyama vya Ford Kenya, Wiper na ANC umeendelea kuzorota katika siku za hivi karibuni tangu Bw Raila Odinga alipojiapishwa Januari 30, na wenzake kukosekana kwa hafla hiyo.

Mbali na hivyo, Bw Odinga hata baada ya kupinga vikali ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta akisema kuwa amenyang’anywa ushindi wake, ameonekana tena kuchukua msimamo wa kibinafsi kwa kufanya mkutano na mpinzani wake, na wawili hao kuafikiana kufanya kazi pamoja, ili kuunganisha nchi.

Maelezo kamili ya mkataba wa wawili hao ungali kitendawili ambacho waliokuwa vinara wenza wameshindwa kukitegua huku Wakenya pia wakishindwa kubaini ikiwa kuna njama nyingine hasa ya kisiasa kando la kilichowekwa wazi.