ODM yaonya wabunge wake dhidi ya kunaswa na Ruto
Na MOHAMED AHMED
CHAMA cha ODM kimetishia kuadhibu wanachama wake waliotangaza watamwunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022.
Hii ni kufuatia tangazo la Jumanne la Mwenyekiti wa Kundi la Wabunge wa Pwani Suleiman Dori (Mbunge wa Msambweni), Badi Twalib (Jomvu) na Benjamin Tayari (Kinango) kuwa watamwunga mkono Bw Ruto.
Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna alisema Jumatano kuwa hatua ya wabunge hao ni kejeli kwa maamuzi ya Baraza la Kitaifa la Chama (NEC).
Bw Sifuna alisema licha ya kuwa ODM haina nia ya kukandamiza haki za wanachama wake kujieleza, wale ambao wanatangaza kuunga mkono wagombeaji wa 2022 wanakiuka maamuzi na miongozo ya chama hicho.
Alisema ODM kupitia kwa NEC kilipitisha maamuzi katika mkutano uliofanywa majuzi kuweka kipaumbele kwa muafaka wa kuleta umoja ulioanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Raila Odinga.
Aliongeza kuwa Bw Odinga pia amekuwa akiambia wanachama wake mara kwa mara wakome kujadili masuala ya siasa za 2022.
“Kinachoshangaza zaidi ni kuwa baadhi ya wale wanaojihusisha katika kampeni hizi za mapema kwa Ruto ni wanachama wa NEC ambao wanafaa kufuata maamuzi yake,” akasema Bw Sifuna kwenye taarifa.
Kulingana naye, chama hicho kinawazia kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wanachama hao kama wataendelea kukiuka mwongozo uliotolewa na kiongozi wa chama.
Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni yaliyohudhuriwa na Bw Ruto katika uwanja wa Baraza Park, Kaunti ya Kwale mnamo Jumanne, wabunge hao walisema watamuunga mkono naibu wa rais kwa kuwa yeye pekee ndiye anayeweza kutatua changamoto zinazokumba jamii ya Wapwani na kuwaletea maendeleo.
Bw Dori alisema ifikapo 2022, eneo hilo lazima liwe ndani ya serikali na hilo litawezekana tu kama watamuunga mkono Bw Ruto.
Kwa upande wake, Bw Tayari alisema watamuunga mkono naibu wa rais ili kuhakikisha Serikali ya Jubilee inaendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo. Wabunge hao ni miongoni mwa wandani wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye pia alitangaza nia yake kuwania urais 2022.
Hata hivyo, wanachama walieleza hisia tofauti kuhusu onyo hilo lililotolewa.
Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya alisema maamuzi ya chama hayawezi kupewa uzito kuliko Katiba inayowapa Wakenya haki ya kujieleza.
“Bw Sifuna amekosa kazi ya kufanya. Inafaa atuache tufanye kazi yetu. Hatuwezi kunyamazishwa na maamuzi ya chama. Bw Ruto ni mshirika katika muafaka wa kuleta umoja na ataendelea kuwa katika mijadala yetu,” akasema Bw Baya.
Bw Twalib alisisitiza kuwa mazungumzo ya umoja yalianzishwa ili kuwezesha watu kushirikiana na viongozi wa vyama vyote na uamuzi wao kumuunga mkono Bw Ruto ni sehemu ya juhudi hizo.
“Kiongozi wa chama chetu alisema muafaka hauhusu 2022 ndiposa tumemchagua Bw Ruto kwa sababu tunajua yeye ndiye atatuongoza siku zitakazofuata 2022. Kama Bw Ruto amedhihirisha kuwa ana uwezo unaotufaa tutazidi kumuunga mkono,” akasema na kuongeza watapambana na hatua za kinidhamu jinsi zitakavyokuja.
Kwa upande wake, Mbunge wa Changamwe, Omar Mwinyi alisema chama kinaongozwa na sheria zinazofaa kufuatwa na kila mwanachama.