Habari

Polisi wampiga risasi babake seneta wa Lamu kwa kutovaa barakoa

May 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

JUMA NAMLOLA na KALUME KAZUNGU

POLISI katika Kaunti ya Laikipia wanalaumiwa kwa kumpiga risasi babake Seneta wa Kaunti ya Lamu, Anwar Loititip kwa madai hakuwa amevaa barakoa.

Kwenye kisa hicho cha Jumapili, maafisa wa polisi wa Doldol walimpiga risasi mguuni mzee David Kiwaka, walipokuwa wakijaribu kumkamata kwa nguvu, kwa madai alihatarisha maisha yake kwa kutojikinga na corona.

Bw Loitiptip alikashifu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi, katika harakati za kuhakikisha masharti ya Wizara ya Afya yanazingatiwa.

“Babangu David Kiwaka amepigwa risasi mguuni na kujeruhiwa vibaya na polisi wa kituo cha Doldol. Walikuwa wakijaribu kumkamata kwa nguvu kwa madai kwamba hakuwa amevaa barakoa. Tumempeleka babangu hospitalini Nanyuki anakoendelea kutibiwa,” akasema.

Seneta huyo anataka uchunguzi wa haraka ili afisa wa polisi aliyehusika na unyama huo akamatwe na kushtakiwa.

Tukio hili lilijiri siku moja baada ya mfanyabiashara mjini Nyeri kulazimishwa atoe hongo, alipofumaniwa na polisi akila bila kuvaa barakoa.

Wiki jana, nyanya mwenye umri wa miaka 93 katika kaunti ya Nyamira alilazimika kuuza kuku wake na kupata pesa za kuwahonga polisi. Ajuza huyo alipatikana na maafisa hao akiwa hana barakoa.

Juhudi hizo za polisi ziliendelea huku jana watu wengine 25 wakiripotiwa kuambukizwa virusi vya corona.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alisema wanaume 23 na wanawake wawili katika kaunti nane walitambuliwa kutoka kwa watu 1,139 waliopimwa.

“Visa hivi 25 vinafikisha idadi ya maambukizi kuwa 912. Kwa jumla tumepima watu 44,851 kufikia sasa,” akasema.

Dkt Aman alitangaza kuwa kaunti tatu – Garissa, Taita Taveta na Meru – ziliripoti kwa mara ya kwanza, jumla visa vitano.

Garissa na Taita Taveta zilikuwa na visa viwili kila moja huku Meru ikiwa na kimoja.

Kajiado ilikuwa na visa sita, Mombasa (5), Nairobi (3), Kiambu (3) na Kwale (3).

Serikali pia ilitangaza kuwa madereva 53 wa matrela kutoka nchi jirani ya Tanzania walipimwa na kupatikana na virusi hivyo wakiwa mpakani. Ingawa serikali ilifunga mpaka wake wana Tanzania na Somalia, wadereva wa kusafirisha mizigo bado wanaruhusiwa kuvuka, kwa sharti wawe wamepimwa na kuwa hawajaambukizwa.