Rais Kenyatta aelekea Amerika kukutana na Trump
NA PSCU
RAIS Uhuru Kenyatta ameondoka nchini kwa ziara rasmi jijini Washington DC, Amerika, ambapo anatazamamiwa kukutana na Rais Donald Trump mnamo Agosti 27.
Ndege aliyosafiria Rais na ujumbe wake iliondoka Uwanja wa Ndege wa Kimatifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) muda mfupi baada ya saa sita usiku Jumamosi.
Maafisa wakuu serikalini wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na Mkuu wa Majeshi Jemedari Samson Mwathethe walimuaga Rais Kenyatta katika uwanja huo.
Akiwa nchini Amerika, Rais Kenyatta atafanya mashauriano na mwenyeji wake Rais Trump kuhusiana na masuala ya biashara na usalama humu nchini.
Kwa miaka mingi sasa, Kenya imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika udumishaji amani na usalama katika eneo la Mashariki mwa Afrika, eneo la Maziwa Makuu na Upembe wa Afrika, ambapo Kenya imekuwa katika msitari wa mbele kurejesha amani katika nchi ya Sudan Kusini.
Huko nchini Somalia, vikosi vya majeshi ya Kenya vinashiriki katika mapambano dhidi ya kundi la magaidi la Al Shabaab chini ya shirika la AMISOM.
Mbali na masuala ya kibiashara na usalama, Rais Kenyatta na Rais Trump watajadiliana kuhusu njia za kuimarisha uhusiano bora kati ya nchi hizi mbili wakizingatia maadili ya kidemokrasia na uelewano.
Mkutano kati ya viongozi hawa wawili unafanyika wakati unaofaa huku Rais Kenyatta akitekeleza mipango ya kuboresha biashara na uwekezaji nchini kupitia Ajenda Nne Kuu za maendeleo.
Aidha, Kenya inanufaika zaidi na mipango ya kibiashara kati yao muhimu zaidi ukiwa ni mkataba wa AGOA ambao Rais Kenyatta atashauriana upya na Rais Trump.
Uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili umeisaidia Kenya kuthibiti uchumi wake na kudumisha usalama, kutoa huduma bora za afya, elimu , kuimarisha utawala wa sheria na utekelezaji wa kanuni za kidemokrasia.
Mkutano kati ya Rais Kenyatta na mwenyeji wake Trump ni hatua bora ya kuimarisha sekta za utalii na za safari za ndege kwani mkutano kati yao unafanyika majuma machache tu kabla ya kuzinduliwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka uwanja wa JKIA hadi jijini New York mwezi Oktoba 2018.
Hapo Agosti 24, Waziri wa Mashauri ya nchi za Kigeni Dkt Monica Juma ambaye tayari alitangulia Marekani, alifanya mashauriano na mwenyeji wake Michael Pompeo kabla ya mkutano kati ya marais hawa wawili.