Referenda yaja, Uhuru adokezea Wakenya
Na VALENTINE OBARA
RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi alidokeza kuunga mkono marekebisho ya Katiba ili kuwe na nafasi zaidi za uongozi serikalini.
Pendekezo hilo limekuwa likipigiwa debe na Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, huku likipingwa na wandani wa Naibu Rais William Ruto.
Akihutubu jana katika eneo la Ahero, na baadaye katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Mamboleo, Kaunti ya Kisumu, Rais alisema kuwa walipoweka muafaka wa maelewano Machi 9 na Bw Odinga, walikubaliana kutafuta jinsi ya kuepusha umwagikaji damu nchini kila uchaguzi wa urais unapofanywa ambapo kila jamii hutaka mtu wao awe mamlakani huku jamii nyingine zikiachwa nje.
Kwa msingi huu, alisema wanatafuta suluhisho la kuepusha mshindi wa urais kutwikwa mamlaka yote ya uongozi.
“Hii siasa ya taifa letu la Kenya ambayo kila saa ni siasa ya mashindano, wengine wanaingia serikalini na wengine wanabaki nje, hatutaki mashindano aina hiyo. Tunataka mashindano ambayo yanatuwezesha kuhakikisha kila jamii, kila Mkenya ataona serikali ni yake. Hiyo ndiyo njia ya kuleta amani na maendeleo ya kudumu,” akasema.
Pendekezo la ODM ni kwamba, katiba irekebishwe ili kuwe na nafasi ya waziri mkuu na manaibu wake na rais awe akichaguliwa na Wabunge.
Wakati huo huo, Rais Kenyatta alisisimua wafuasi wa upinzani kwa kutangaza Bw Odinga yuko ndani ya serikali.
Tangu wawili hao walipoweka muafaka, baadhi ya viongozi wamekuwa wakitaka kujua kama Bw Odinga alipewa kiti serikalini ingawa yeye husisitiza angali katika upinzani.
“Jakom (Bw Odinga) sasa tunasema yuko ndani ya serikali. Huwa tunashauriana na tunaongea kuhusu mambo yanayohusu wananchi,” akasema alipohutubia wananchi waliomshangilia katika eneo la Ahero.
Alikuwa Kisumu kuzindua mpango wa utoaji huduma bora za afya kwa wananchi kwa bei nafuu, ambayo ni mojawapo ya nguzo nne kuu za maendeleo anazolenga kutekeleza kabla akamilishe hatamu yake ya pili iliyo ya mwisho ya uongozi mnamo 2022.
Awamu ya kwanza ya mpango huo itatekelezwa Kisumu, Nyeri, Isiolo na Machakos kabla kusambazwa hadi kaunti zingine zote.
Bw Odinga aliambia wakazi kuwa walielewana na rais kurudisha umoja wa Kenya jinsi ilivyokuwa kabla taifa lilipopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa wakoloni.
Kwa upande wake, Bw Ruto alisifu umoja ulioletwa na muafaka wa wawili hao na kusema viongozi wote wamekubali kuzika uhasama uliokuwepo awali.
“Mkiona Uhuru Kenyatta na muone Waziri Mkuu Raila na muone ‘hustler’ hapa katikati yao mjue mambo ni sawa. Sisi sote tumekubaliana tutatembea pamoja na kuunganisha Wakenya,” akasema.
Rais Kenyatta aliwasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu dakika chache baada ya saa tano asubuhi alipolakiwa rasmi na Bw Odinga pamoja na Bw Ruto, miongoni mwa viongozi wengine.
Ziara hiyo ilikuwa ya kwanza ya Rais Kenyatta Kisumu tangu muafaka huo maarufu na Bw Odinga.
Leo wawili hao wanatarajiwa katika Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga kilicho Bondo, Kaunti ya Siaya, ambako ni nyumbani kwa Bw Odinga.